Habari

Imewekwa: Apr, 18 2025

Utekelezaji wa Mradi wa Maji wa Mto Kiwira Mbeya Washika Kasi

News Images

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mbeya (Mbeya UWASA) imepokea sehemu ya bomba ya utekelezaji wa mradi wa Maji toka chanzo cha mto Kiwira.

Hafla ya mapokezi imeongozwa na Mhe. Dkt. Tulia Ackson Mbunge wa Jimbo la Mbeya Mjini, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Rais wa Mabunge Duniani

Dkt. Tulia amemshukuru Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutoa Sh. 119 Bilioni kwa ajili ya kutekeleza mradi huo ambao utamaliza changamoto ya upatikanaji wa huduma ya maji katika Jiji la Mbeya, Mji wa Mbalizi na Vijiji vinavyopitiwa na mradi huu. Pia, amemshukuru Mhe.Jumaa Aweso (Mb) Waziri wa Maji kwa uongozi makini katika Sekta ya maji.

Mhe. Tulia ameipongeza Mamlaka ya Maji Mbeya kwa kazi nzuri ya kusimamia huduma ya maji ikiwemo usimamizi wa utekelezaji wa mradi wa maji chanzo cha Mto Kiwira.

Dkt Tulia amemtaka Mkandarasi wa mradi kutekeleza mradi kwa kuzingatia viwango na kukamilisha mradi ndani ya muda uliopangwa.

Vilevile Dkt. Tulia ametoa rai kwa Wananchi kutunza mazingira na vyanzo vya maji ili huduma ya maji iwe endelevu.

Akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi wa maji wa kimkakati kutoka chanzo cha mto Kiwira CPA. Gilbert Kayange Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Maji Mbeya amesema kuwa Mamlaka inatarajia kupokea bomba 3, 109 zenye urefu wa Mita 12 kila moja ambazo zitalazwa kwa umbali wa Kilomita 37.24 kutoka kwenye chanzo hadi eneo la Forest mpya Jijini Mbeya ambapo kunajengwa tanki la Lita Milioni 5.

CPA. Kayange amesema bomba hizo ni za chuma zenye kipenyo milimita 1,200, zimetengenezwa kwa kuzingatia viwango vya ubora na kwamba zina uwezo wa kudumu kwa zaidi ya miaka 50.

Mradi wa maji wa mto Kiwira utazalisha maji lita milioni 117 kwa siku na utahudumia Wananchi zaidi ya milioni moja laki tano wa Jiji la Mbeya, Mji wa Mbalizi na Vijiji vinavyopitiwa na mradi.