Habari

Imewekwa: Sep, 30 2025

Hungary Kushirikiana na Tanzania Katika Mradi wa Maji wa Biharamulo

News Images

Serikali ya Tanzania imefanya majadiliano na Hungary kuhusu utekelezaji wa Mradi wa Usambazaji Maji wa Biharamulo, utakaotekelezwa kwa mkopo wa masharti nafuu kutoka Serikali ya Hungary.

Majadiliano hayo yalifanyika jijini Dar es Salaam katika ofisi ndogo za Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, yakiongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahomud Thabit Kombo, kwa upande wa Tanzania, na Waziri wa Mambo ya Nje na Biashara wa Hungary, Mhe. Peter Szijjarto, kwa upande wa Hungary.

Akizungumza katika kikao hicho, Balozi Kombo alisema mradi huo ni sehemu ya jitihada za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuhakikisha jamii inaondokana na changamoto ya upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama. Alibainisha kuwa mradi huo utatumia teknolojia za kisasa kusafirisha maji kutoka Ziwa Victoria na kuyatibu kabla ya kuwafikishia wananchi.

Kwa upande wake, Mhe. Szijjarto alisema Tanzania ni mshirika muhimu wa maendeleo kwa Hungary, na uhusiano huo umewezesha kufanikisha mradi huo wa masharti nafuu. Alisisitiza kuwa mradi huo utakuwa mchango mkubwa katika kulinda afya za wananchi na kuimarisha maendeleo ya kijamii na kiuchumi, si Tanzania pekee bali pia katika kanda ya Afrika kwa ujumla.

Ziara ya Waziri Szijjarto na majadiliano haya yanabeba umuhimu mkubwa katika kuimarisha ushirikiano wa kidiplomasia na kiuchumi kati ya Tanzania na Hungary, hususan katika sekta ya maji na huduma za kijamii.