Habari
Wizara ya Maji Yafanya Kikao cha Majadiliano Kuhusu Teknolojia ya Onyo la Mapema

Wizara ya Maji imefanya kikao cha majadiliano na Shirika la GSMA kuhusu ushirikiano katika teknolojia ya kisasa katika kuimarisha mifumo ya onyo la mapema nchini, Cell Broadcast.
Majadiliano yamefanyika kwa njia ya mtandao, na kuhudhuriwa na wataalamu wa Wizara ya Maji pamoja na wataalamu wa GSMA.
Mhandisi Peter Kishiwa katika majadiliano amesema njia bora za kuanzisha na kueneza teknolojia ya onyo la mapema inalenga kuhakikisha wananchi wanapata taarifa muhimu za tahadhari kwa haraka katika maeneo yanayokabiliwa na hatari za ukame, mafuriko na majanga mengine yanayosababishwa na mabadiliko ya tabianchi. Pia, maeneo ya huduma ya majisafi, mabwawa na usimamizi wa vidakio vya maji.
“Teknolojia ya Cell Broadcast itarahisisha kufikia wananchi haraka na kwa usahihi, huku ikiboresha mifumo ya tahadhari ya kitaifa. Hii itasaidia kupunguza hasara za maisha na mali, na kuongeza ustahimilivu wa jamii dhidi ya majanga,” Mhandisi Kishiwa amesema.
Wataalamu wa GSMA yenye makao makuu jijini Casablanca, Morocco wameeleza kwamba Tanzania inaweza kutumia mfumo huo kama chombo chenye nguvu cha kueneza tahadhari kwa jamii zenye hatari kubwa, na wakisisitiza kuwa ushirikiano kati ya Sekta ya Maji na GSMA unalenga kuendeleza mafunzo kwa watendaji wa Serikali na wadau wanaohusika na majanga, na kuimarisha mifumo ya tahadhari ya kitaifa.
Majadiliano yamehusu miradi ya majaribio katika baadhi ya maeneo hatarishi, mbinu za kutumia kufikia idadi kubwa ya wananchi kwa wakati mmoja na namna ya kuhakikisha ujumbe unafika kwa wale wasio na simu za kisasa. Wizara ya Maji imesema kuwa teknolojia hiyo ni ya kisasa kuhakikisha usalama wa wananchi na kuimarisha utawala bora wa tahadhari za majanga.
Cell Broadcast ni nyenzo ya kisasa, yenye uwezo wa kufikia idadi kubwa ya wananchi kwa wakati mmoja, jambo litakalosaidia kuunda taifa linalojitahidi kudhibiti majanga kabla hayajatokea.