Habari

Imewekwa: Sep, 30 2025

Katibu Mkuu Maji Awataka Wahandisi Kuchangamkia Fursa za Utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050

News Images

Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mhandisi Mwajuma Waziri amewataka wahandisi nchini kuchangamkia fursa zilizopo za kufanikisha malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, inayolenga kulifikisha taifa katika uchumi wa kipato cha kati cha juu.

Kauli hiyo imetolewa wakati Mhandisi Mwajuma akiwasilisha mada yenye kichwa “Nafasi ya Uhandisi katika Utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050” kwenye maadhimisho ya 22 ya Siku ya Wahandisi Tanzania, yaliyoongozwa na kaulimbiu isemayo: “Wajibu wa Wahandisi Kuelekea Dira ya Maendeleo 2050”, jijini Dar es Salaam.

Mhandisi Mwajuma amebainisha kuwa Sekta ya Maji ni nguzo muhimu ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi, ikihitaji ubunifu wa kihandisi ili kufanikisha miradi mikubwa kama ujenzi wa Gridi ya Taifa ya Maji, mabwawa makubwa, na miundombinu ya umwagiliaji yenye ufanisi wa matumizi ya maji.

Ameongeza kuwa sekta hiyo inakabiliwa na changamoto zinazohitaji mchango wa wahandisi, ikiwemo gharama kubwa za umeme katika miradi ya maji, uwezo mdogo wa ndani katika ujenzi wa miradi mikubwa, na hitaji la viwanda vya ndani vinavyotengeneza dira na vifaa vya maji.

“Taaluma ya Uhandisi ina fursa mpya za miradi ambazo zinaweza kutekelezwa, ikiwemo mifumo ya maji smart isiyojumuika kwenye gridi, uzalishaji wa maji kwa kutumia nishati ya jua kwa jamii za pwani na visiwa, suluhisho la kutengeneza rasilimali kutoka majitaka, na uhandisi wa kustahimili mafuriko,” Mhandisi Mwajuma amesema.

Ameongeza kuwa Wizara ya Maji imeanza utekelezaji wa Gridi ya Taifa ya Maji, ambapo miradi mikubwa tayari imekamilishwa au inaendelea kutekelezwa katika vyanzo vya maji vya uhakika kama vile maziwa, mito, na mabwawa makubwa, jambo linalowapa wahandisi nafasi ya kushiriki kikamilifu katika kufanikisha maendeleo ya sekta hiyo.

Aidha, amesisitiza kuwa maji ni sekta wezeshi na kichocheo cha mageuzi, hivyo sekta hii imepewa umuhimu mkubwa katika kufanikisha malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, ili kuhakikisha taifa lina usalama wa maji na maendeleo endelevu ya kijamii na kiuchumi.