Habari
RUWASA na EACOP Zafikia Makubaliano Kufikisha Huduma ya Maji Wakazi 27,000

Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) umesaini mkataba na Shirika la Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) kwa ajili ya ujenzi wa Mradi wa Maji katika Vijiji Tisa (9) wenye thamani ya zaidi ya Shilingi Bilioni 1.4 katika mikoa ya Manyara na Dodoma.
Hafla hiyo imefanyika jijini Dar es Salaam, Mgeni rasmi alikuwa ni Mkurugenzi Msaidizi Uendeshaji na Matengenezo, Mhandisi Charles Mafie akimwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mhandisi Mwajuma Waziri.
Kwa mujibu wa makubaliano hayo, EACOP itatoa fedha za kutekeleza mradi kupitiia Uwajibikaji kwa Jamii, “Corporate Social Responsibility” huku RUWASA ikihusika na utekelezaji wa mradi ili kuhakikisha upatikanaji wa huduma ya majisafisi na salama kwa zaidi ya wakazi 27,000 wa vijiji vya Kaloleni, Songolo (Chemba) na Mtiryangwi (Kondoa) mkoani Dodoma pamoja na Ndaleta, Mwitikila, Njoro, Napilikunya, Masusu na Kitwai B katika Wilaya za Kiteto, Hanang’ na Simanjiro mkoani Manyara.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mhandisi Mafie amempongeza RUWASA na EACOP kwa makubaliano hayo na kuwaasa watendaji wa RUWASA kutumia fursa hiyo adhimu kwa ufanisi na kusimamia utekelezaji wa mradi huo vizuri, ili fedha zilizotolewa na wadau ziweze kuleta matokeo chanya.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa RUWASA, Mhandisi Ruth Koya, ameishukuru EACOP kwa kuiamini RUWASA na kuelekeza fedha katika miradi ya maji vijijini. Akifafanua kuwa mradi huo utasaidia kupunguza idadi ya vijiji ambavyo vinakosa huduma ya majisafi na kuomba wadau waendelee kusaidia vijiji vingi zaidi pale watakapokuwa na fursa ya kufanya hivyo.
Akizungumza kuhusu hali ya huduma ya maji vijijini, Mkurugenzi Mkuu wa RUWASA, Mhandisi Wolta Kirita, amesema kuwa taasisi hiyo tayari imetekeleza zaidi ya miradi 3,000, na mradi huu utasaidia kufanikisha juhudi za kufikisha majisafi katika takribani vijiji 1,500 ambavyo havijafikiwa na huduma hiyo nchini.
Naye Mtendaji Mkuu wa EACOP Tanzania, Geofrey Mponda, ametoa pongezi kwa kazi nzuri inayofanywa na RUWASA katika kutoa huduma ya maji vijijini, jambo lililowavutia kuingia makubaliano haya kwa kuamini kwamba fedha zitakazotolewa zitasaidia wananchi kupata huduma muhimu ya majisafi na kuboresha maisha yao.