Habari

Imewekwa: Jan, 25 2024

Huduma ya majisafi ilivyopunguza zaidi ya asilimia 50 ya magonjwa ya kuhara Katavi.

News Images

Julai 24, 2022 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango alizindua mradi wa maji wa Sibwesa wilayani Tanganyika mkoani Katavi. Mradi huo unahudumia zaidi ya wakazi wapatao elfu nane wa kata ya Sibwesa. Katika uzinduzi huo, Naibu Waziri wa Maji Mhe. Mhandisi Maryprisca Mahundi (Mb) alimwakilisha Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso (Mb).

Baadhi ya maelekezo na maagizo aliyoyatoa Makamu wa Rais ilikuwa ni pamoja na kuhakikisha mradi huo unakuwa msaada wa kupunguza adha ya changamoto ya huduma ya majisafi na salama kwa wananchi ikiwemo kuwaepusha na magonjwa ya mlipuko yanayosababishwa na matumizi ya maji yasiyo salama.

Ikiwa ni takribani miezi 18 tangu mradi huo uzinduliwe, mradi umeleta mabadiliko makubwa katika eneo la afya ya jamii. Dkt. Miriam Lulandala ni Mganga mfawidhi wa Kituo cha Afya cha Sibwesa ambacho kinahudumia wananchi wengi ambao wananufaika na huduma ya maji kutoka mradi huo.

Anasema baada ya Serikali kusambaza mabomba ya huduma ya maji kutoka katika mradi wa maji Sibwesa magonjwayanayosababishwa na matumizi ya maji yasiyo salama yamepungua kutoka wastani wa wagonjwa 80 kwa mwezi kwa mwaka 2020 wakati ambao mradi huo ulikuwa haujaanza kutoa huduma hadi kufikia wagonjwa 34 kwa mwezi kwa mwaka 2023 ambapo mradi umesambazwa na kufikishwa katika makazi ya wananchi wengi.

Mradi huo ulianza kutoa huduma mapema mwezi Aprili 2021 mwaka ambao matatizo yanayotokana na magonjwa ya hayo yaliyoelezwa na mtaalamu wa afya ya binadamu yalianza kupungua.

Dkt. Miriam anasema mwaka 2020 kuanzia Julai hadi Desemba kituo hicho kilipata wagonjwa wa magonjwa ya yanayosabishwa na kunywa maji yasiyo salama inayofikia 477 ambayo ni sawa na asilimia 79.5 kwa mwezi. Mwaka 2021 mradi ulipoanza kutoa huduma wagonjwa wa aina hiyo kwa miezi hiyo sita walipungua na kufikia 373 sawa na asilimia 62.1 wakati mwaka 2022 mradi ulipoendelea kupanuliwa na kuwafikia wananchi wengi, kituo hicho kilipokea wagonjwa 274 sawa na asilimia 46.

Baada ya miundombinu ya mradi huo kusambazwa na kuwafikia wakazi wengi zaidi, hali imebadilika kwa kiasi kikubwa. Anasema mwaka 2023 kuanzia mwezi Julai hadi Desemba takwimu za afya za kituo kituo zinaonyesha wagonjwa wa aina hiyo waliopokelewa na kuhudumiwa ni 203 tu, ambayo ni sawa na wastani wa wagonjwa 34 kila mwezi.

“Hili ni suala la kumshukuru la kumshukuru Mungu kwa huduma yam aji kwa wananchi. Ni sadaka kubwa ambayo serikali imeamua kuwapa wananchi wa Sibwesa ili kulinda afya zao”. DKt. Miriam anasema huku akiiomba serikali iendelee na jitihada hizi ili kuhakikisha maeneo yote nchini yanafikiwa na huduma ya majisafi na salama ili kulinda afya za wananchi.

Anasema kabla ya kupata huduma hii wananchi walikuwa wakitumia maji kutoka madimbwi na visima vya kienyeji ambavyo walikuwa wakitumia pamoja na mifugo hali ambayo ilikuwa ikisababisha kupata maradhi ya mbalimbali yasababishwayo na matumizi yam aji yasiyokuwa salama.

Anasema changamoto nyingine iliyokuwa ikisababisha ongezeko la magonjwa, ni kwa akina mama waliokuwa wakienda kituoni kupata huduma ya kujifungua walikuwa wakilazimika kuondoka na nguo zao chafu kwenda kufanyia usafi nyumbani hali ambayo ilikuwa ikisababisha maambukizi mapya ya magonjwa katika makazi yao.

“Si huduma ya maji ya usafi tu, sasa hivi hata huduma ya maji ya kunywa kwa watoto na wazazi ipo na maji hayo ni safi na salama hivyo afya imeendelea kuimarika kwa kiasi cha kutosha katika maeneo yanayonufaika na mradi huu.” Dkt. Miriam anasema

Ushuhuda huu wa Dkt. Miriam unaungwa mkono na Shamira Kiwele mkazi waSibwesa. Shamira anasema ni Mama wa Watoto wawili ambaye mtoto wake wa pili alijifungilia hapo kituoni katika kipindi ambacho hakukuwa na huduma ya majisafi na salama.

Anakumbuka yaliyotokea akisema ndugu zake waliomsindikiza kumuuguza ilibidi wahangaike kupata maji ya kwa ajili ya usafi. Anashukuru kwamba pamoja na usumbufu huo wa huduma ya majisafi na salama, wahudumu wa afya katika kituo hicho walikuwa wakipambana sana kuhakikisha mzazi anaendelea kuwa salama wakati wote.

Anashukuru huduma hiyo kuingia katika maeneo hayo ikiwepo majumbani kwani licha ya kupata huduma ya majisafi na salama kwa wazazi shughuli za kiuchumi na kijamii zimeimarika. Ratiba ya kazi za kifamilia imekaa vizuri kwani ratiba muhimu ya kusafiri umbali mrefu kutafuta maji imeisha.

Diwani wa kata hiyo Mhe. Deusi Masunga anasema sasa malalamiko aliyokuwa akikutana nayo kutoka kwa wananchi yamekwisha. Anaiomba serikali iendelee kuwekeza katika huduma za kijamii na anatoa shukrani kwa Wizara ya Maji kwa kuhakikisha huduma hiyo ya majisafi na salama inafika katika vituo vyote vya huduma za kijamii katika kata yake.

Anasema maji hayo yamewezesha kuanza ujenzi ili kupanua kituo hicho cha Afya cha Sibwesa kwa sababu changamoto ya huduma ya maji ya ujenzi haipo tena.

Meneja wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) wilaya ya Tanganyika Mhandisi Alkam Sabuni anasema wanatambua umuhimu wa huduma ya majisafi kwa jamii hasa katika suala la afya. Kwa kutambua hilo walihakikisha wanafikisha huduma ya majisafi katika vijiji vyote vilivyoko katika kata hiyo si kwa wananchi tu bali wamehakikisha maji hayo yafikishwa katika vituo vyote vya huduma za kijamii.

“Kata hii ya Sibwesa inazo Taasisi za Umma sita na zote tumezifikishia huduma ya majisafi na salama”Sabuni anasema na kusisitiza kuwa wameaminiwa kufanya kazi, hivyo ni lazima watimize wajibu wao.

“Tumeapa na tumeaminiwa kuhakikisha tunafikisha huduma kwa wananchi. Hilo ndilo tunalolizingatia na tunashukuru Serikali yetu pamoja na uongozi wa ngazi ya juu ya wizara na RUWASA makao makuu wanatuunga mkono.” Anasema Alkam Sabuni

Anasema Wilayaya Tanganyika anayoihudumia ina vijiji 55 vyenye wakazi wapatao 375,000. Vijiji takribani 39 vyenye wakazi wapatao 330,000 vimefikiwa na huduma ya majisafi na salama na hivyo kufanya asilimia ya wananchi wanaopata huduma hiyo kufikia 81.

Anasema kwa aina ya miradi inayoendelea kutekelezwa kwa fedha ya Serikali katika wilaya hiyo matumaini ni kuwa mwaka wa fedha 2024/2025 huduma ya majisafi na salama itafikia asilimia 92. Jambo walilozingatia, ni kwa Taasisi zote za umma katika vijiji vyote 39 walivyovifikia wamepelekewa huduma ya majisafi na salama hali ambayo imewezesha usalama wa kiafya kwa watu wengi wa wilaya ya Tanganyika.