Habari
Huduma ya Maji Inazidi Kuimarika Katavi
Huduma ya maji mkoani Katavi inazidi kuimariki baada ya miradi ya maji iliyokuwa ikitekelezwa kukamilika na wananchi kuanza kupata huduma hiyo karibu na makazi yao.
Meneja wa Wakala wa Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) mkoani Katavi Mhandisi Peter Mugula amesema kuimarika huko ni matokeo ya jumla ya miradi ya maji 14 kukamilika. Ameongeza kuwa miradi 24 ipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji na inatarajiwa kukamilika kabla ya Desemba 2020.
Mhandisi Mugula amesema hadi mwezi Agosti 2020 asilimia 62 kutoka asilimia 51 ya wakazi waishio vijijini tayari walishapata huduma ya maji, na mjini asilimia ya ilipanda hadi 75 kutoka asilimia 40 ya wananchi waliokuwa wakipata huduma ya maji. Amefafanua kuwa mabadiliko hayo yametokana na baadhi ya miradi kukamilishwa na wataalam wa sekta ya maji kwa utaratibu wa force account.
Ameainisha kuwa miradi ya maji ya mjini inasimamiwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira (MUWASA), ambapo hivi sasa mamlaka hiyo imeanza maandalizi ya kujenga mradi wa maji wa Kanoge II utakaozalisha maji mita mita za ujazo 1,200. Mradi wa Kanoge utaimarisha zaidi upatikanaji wa maji hadi kufikia mita za ujazo 8,700 hivyo kufanya kiwango cha upatikanaji maji kufika asilimia 87.
Mhandisi Mugula amesema kuwa lengo ni kuwafikia wananchi wote katika huduma ya maji na hakuna atakayeachwa. Takwimu za sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012 inaonyesha kuwa mkoa wa Katavi una jumla ya watu 564, 604 na mwaka 2018 mkoa huo ulikadiriwa kuwa na idadi ya watu 738, 237.
Kitengo cha Mawasiliano

