Habari
Mhandisi Mwajuma Amtaka Mkandarasi Kufanya Kazi Saa 24 Kukamilisha Mradi wa Miji 28 Tanga

Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mhandisi Mwajuma Waziri, amemuagiza mkandarasi anayetekeleza Mradi wa Maji wa Miji 28 katika miji ya Korogwe, Handeni, Muheza na Pangani kufanya kazi usiku na mchana ili kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati na kuanza kutoa huduma kwa wananchi.
Akizungumza wakati wa ziara ya kukagua maendeleo ya mradi huo, Mhandisi Mwajuma amesema kuwa hatua iliyofikiwa hadi sasa ni ya kuridhisha, ambapo ujenzi umefikia asilimia 70. Hata hivyo, amesisitiza kuwa kasi ya utekelezaji inapaswa kuongezwa, hususan katika eneo la ujenzi wa mtambo wa kuchuja maji, ambalo kwa sasa halina changamoto zozote zinazoweza kusababisha ucheleweshaji.
“Lazima mkandarasi aongeze nguvu na kutumia muda wote uliopo kuhakikisha mradi huu unakamilika kwa wakati. Agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ni wazi: miradi ya maji ikamilike kwa muda uliopangwa, bila visingizio. Wizara haitatoa nafasi ya kuongeza muda wa utekelezaji,” Mhandisi Mwajuma amesema.
Mradi wa Miji 28 unatarajiwa kukamilika ifikapo Desemba 2025 na unatarajiwa kuongeza uwezo wa kuzalisha lita milioni 51 za maji kwa siku, hatua itakayosaidia kuboresha upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama kwa wakazi wa maeneo husika.
Aidha, Katibu Mkuu Mhandisi Mwajuma Waziri amebainisha kuwa mradi huo unatumia chanzo cha maji cha Mto Pangani na ni sehemu ya utekelezaji wa Gridi ya Taifa ya Maji, mkakati wa kimkakati wa Serikali unaolenga kutumia vyanzo vya uhakika vya maji ili kuongeza upatikanaji wa huduma kwa wananchi kote nchini.
Ameongeza kuwa kukamilika kwa mradi huu kutachangia si tu kupunguza changamoto za upatikanaji wa maji majumbani, bali pia kuongeza tija katika shughuli za kijamii na kiuchumi ikiwemo elimu, afya na biashara.
“Wananchi wanatarajia kuona matunda ya mradi huu. Hatutakubali ucheleweshaji, tunataka ukamilike kwa viwango na muda uliopangwa ili uweze kubadilisha maisha ya watu wetu,” Mhandisi Mwajuma amesisitiza.