Habari

Imewekwa: Jan, 31 2024

Chuo cha Maji kinazalisha wasomi wenye weledi - Dkt. Kikwete

News Images

Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete amekipongeza Chuo cha Maji kwa kuwa na Mfumo wa elimu ambao unawezesha wahitimu wake kujiajiri au kuajiriwa kwa urahisi zaidi.

Pongezi hizo amezitoa leo katika maadhimisho ya Miaka 50 ya Chuo hicho ambayo yalienda sambamba na Ufunguzi wa Kongamano la Tatu la Kimataifa la Kisayansi la Maji.


“Mfumo wa elimu mnaotumia yaani Competence Based Approach umesaidia kufanya wahitimu wa Chuo cha Maji kuweza kujiajiri au kuajiriwa kwa urahisi zaidi hivyo endeleeni kuboresha mazingira ya kufundishia na kufundisha ili wahitimu waweze kufanya kazi kwa ushindani zaidi ndani na nje ya nchi.”

Amesisitiza chuo hicho kihakikishe kuwa mitaala yake ya mafunzo inalenga pia utatuzi wa Mabadiliko ya Tabianchi na kufanya wahitimu wawe na ujuzi na weledi wa kukabiliana na kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi kwani mabadiliko hayo yameendelea kuwa changamoto kubwa katika kufikia malengo endelevu.

Amempongeza Mkuu wa Chuo hicho Dkt. Adam Karia kwa ubunifu na jinsi anavyoongoza Taasisi kwa kufanya maboresho na mageuzi makubwa yanayolenga kukifanya chuo kiwe bora zaidi katika kutekeleza majukumu yake ya sasa na kwa siku zijazo.

Amesema bunifu mbalimbali ambazo zimefanywa na Chuo kwa miaka ya hivi karibuni ni ishara tosha kuwa chuo kimedhamiria kufanya mapinduzi makubwa ya kifikra ili kuweza kuhudumia watanzania vizuri zaidi.


Naye Naibu Katibu Mkuu Wizara Maji Mhandisi Mwajuma Waziri akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara Profesa jamal Katundu amesema Wizara ya Maji ipo katika mchakato wa kuandaa Sera ya Taifa ya Maji (National Water Policy) baada ya Sera iliyopo (NAWAPO -2002 -2022) kuisha muda wake. Amewahakikishia wananchi kuwa Sera Mpya itakapokamilika itapunguza changamoto nyingi zinazoigusa sekta ya maji.


Kongamano la Kimataifa la Kisayansi la Maji mwaka huu linafanyika jijini Dar es Salaam likiwa na kaulimbi isemayo; Maji na Usafi wa Mazingira katika Ulimwengu wa Mabadiliko (Water and Sanitation in a Changing World)