Habari
Changamoto ya Huduma ya Majisafi Dar es salaam Mwisho 2023

Naibu Waziri wa Maji Mhe. Mhandisi Maryprisca Mahundi (Mb) amewahakikishia wananchi wanaopata huduma ya majisafi na salama kupitia Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es-salaam (DAWASA) ambao hawajafikiwa na huduma hiyo kuwa ndani ya miaka miwili maeneo yote yanayotakiwa kuhudumiwa yatafikiwa.
Ameyasema hayo wakati akikagua maboresho yaliyofanywa katika mitambo ya kuzalisha maji ya Ruvu Juu na Ruvu Chini
Amesema maboresho hayo yamelenga kuhakikisha changamoto ya upatikanaji wa majisafi na salama katika maeneo yanayohudumiwa na DAWASA inaisha.
“ Maeneo yote mabayo hayajafikiwa na maji tuendelee kuwa na subira. Tulikotoka ni mbali. Tunakokwenda ni karibu. Muda si mrefu maeneo yote yatapata maji bombani.” Mahundi amesema.
Ameongeza kwa sasa DAWASA inatoa huduma ya maji kwa asilimia 92 katika maeneo yake, na hadi kufika mwaka 2023 maeneo yote yatakuwa yamefikiwa.
Awali akitoa taarifa ya hali ya huduma ya majisafi na salama Mkurugenzi wa Uzalishaji na Usambazaji Maji wa DAWASA Mhandisi Shaban Mkwanywe amesema mtambo wa Ruvu chini ulifanyiwa maboresho mwaka 2013 na kuwezesha ongezeko la upatikanajni wa Maji kutoka lita milioni 180 kwa siku hadi lita milioni 270 kwa siku wakati ule wa Ruvu Juu Matengezezo yake yalifanyika mwaka 2016 ambapo mtambo huo uliweza kuongeza upatikanaji wa maji kutoka lita milioni 82 kwa siku hadi lita milioni 196 kwa siku.
“Sisi kama DAWASA nia yetu ni kuondoa kabisa tatizo la upatikanaji wa maji katika jiji la Dar es salaam ifikapo mwaka 2023.” Mhandisi Mkwanywe amesema.
Kitengo cha Mawasiliano