Habari
Aweso awataka wamiliki wa mabwawa ya tope sumu kuzingatia usalama

Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso (Mb) amewataka wamiliki wa mabwawa ya tope sumu kuhakikisha wanaweka miundombinu bora ili kuzuia utililishaji wa maji ya sumu katika mazingira. Naibu Waziri, Wizara ya Katiba na Sheria Mhe. Jumanne Sagini (Mb) amesema hayo akimwakilisha Mhe. Aweso katika ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa Usalama wa mabwawa.
Mkutano huu umefanyika jijini Mwanza ukiwahusisha wadau mbalimbali wa mazingira kwa lengo la kupeana maarifa mbalimbali ya uzuiaji wa athari za topesumu katika mazingira ikiwemo matumizi ya kapeti la kuzuia tope sumu kupenya chini ya ardhi.
Amesema kazi iliyofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Daktari Samia Suluhu Hassan ya kutoa huduma ya majisafi kwa watanzania ni kubwa na inatakiwa kulindwa. Amesema ipo miradi ya mabwawa ya maji ambayo yamejengwa sehemu mbalimbali nchini hivyo lazima kuwepo na jitihada za kuhakikisha mabwawa hayo pamoja na mazingira kwa ujumla hayaathiriki.
Mkutano huo umeandaliwa kwa ushirikiano wa Wizara ya Maji na Chamber of Mines ambapo kwa nyakati tofauti Mkurugenzi wa Rasilimali za Maji Dkt George Lugomela pamoja na Mkurugenzi upande wa Chamber of Mines Mhandisi Benjamini Mchwampaka wamesema mkutano huo wa siku tatu utasaidia kwa kiasi kikubwa kuwa na mikakati ya pamoja kuhakikisha usalama wa mabwawa na watumiaji wa huduma ya majisafi wanaendelea kuwa salama.