Habari

Imewekwa: Aug, 30 2021

Aweso Atoa Siku 60 Mradi Kukamilishwa Dodoma

News Images

Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso (Mb) ametoa miezi miwili kwa wataalamu kukamilisha Mradi wa Maji wa Ihumwa - Njedengwa jijini Dodoma.

Waziri Aweso ameelekeza hilo baada ya kukagua na kuona maendeleo mradi huo wa ujenzi unaotekelezwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA).

Amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan ametoa shilingi Bil.2.7 kwa ajili ya Utekelezaji wa Mradi huo kwa lengo la kuhakikisha changamoto ya upatikanaji wa majisafi jijini Dodoma inaisha.

Mradi wa Ihumwa - Njedengwa utahudumia wakazi wa eneo la Njedengwa, Iyumbu, Soko la Ndugai, Stendi ya mabasi, Nyumba 300 (Mwangaza), eneo la FFU na Nzuguni pamoja na kuongeza upatikanaji wa majisafi katika maeneo mengine ya Jiji la Dodoma.

Aidha, amemteua msimamizi wa mradi huo Meneja wa Ufundi wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA), Mhandisi Kashilimu Mayunga kuwa Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji na atapangiwa kituo cha kazi.