Habari

Imewekwa: Apr, 30 2021

Aweso Akutana na Ujumbe Kutoka Wizara ya Maji Zanzibar

News Images

Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso (Mb) leo amekutana na ujumbe kutoka Wizara ya Maji, Nishati na Madini ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.

Akizungumza na ujumbe huo katika kikao kilichofanyika jijini Dodoma, Waziri Aweso amesema Wizara ya Maji Tanzania Bara haitakuwa kikwazo katika kujenga mahusiano mema na Wizara ya Maji, Nishati na Madini Zanzibar katika kuhakikisha wananchi wa pande zote mbili wanapata huduma ya majisafi, salama na yenye kutosheleza.

“Sisi viongozi wa Wizara ya Maji hatutakuwa kikwazo kutoa ushirikiano wa dhati kabisa kuhakikisha tunaijenga nchi yetu, si Tanzania Bara tu bali na Tanzania Visiwani kwa kuhakikisha changamoto za upatikanaji wa majisafi, salama na yenye kutosheleza zinapatiwa ufumbuzi”, Waziri Aweso amesema.

Amesisitiza kwamba Wizara ya Maji Tanzania Bara inakwenda kuleta mabadiliko makubwa katika suala la utunzaji wa vyanzo vya maji, usambazaji maji na kulinda miundombinu ya maji ili iwe endelevu.

“Tunaweza kupeleka huduma ya maji maeneo mbalimbali lakini bila kuvilinda vyanzo vya maji vitapotea”, Waziri Aweso amesisitiza.

Kwa upande wake Katibu Mkuu, Wizara ya Maji Nishati na Madini Zanzibar, Mngereza Miraji Mzee amefurahia kukutana na viongozi wa Wizara ya Maji Tanzania Bara na kusisitiza kwamba changamoto zinazoikumba sekta ya maji zinaweza kutatuliwa pale kunapo kuwepo ushirikiano wa pande zote mbili.

“Hatutaki kufanya makosa kwa sababu zama hizi ni zama za mawasiliano. Tunaweza kujifunza kila upande ili kuepuka makosa yasiyo ya lazima.” Katibu Mkuu, Maji, Nishati na Madini Zanzibar amesema.

Ujumbe kutoka Wizara ya Maji, Nishati na Madini ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar umekuja kubadilishana uzoefu katika usimamizi wa rasilimali za maji chini ya ardhi ambapo kesho tarehe 30 Aprili, 2021 watatembelea eneo la Mzakwe maarufu kama Makutupora, eneo ambalo kuna visima vinavyolisha wakazi wa jiji la Dodoma. Eneo hilo lina uwezo wa kutoa mita za ujazo 62,000 kwa siku.