Habari

Imewekwa: Mar, 09 2026

Wanawake Sekta ya Maji Wang’ara Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani 2026

News Images

Wanawake wa Sekta ya Maji wakiongozwa na Timu ya Wanawake ya Wizara ya Maji pamoja na Taasisi zake wameshiriki kikamilifu katika maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani yaliyofanyika tarehe 8 Machi 2026 katika Mkoa wa Dodoma, wakionesha mshikamano wao katika kuendeleza usawa wa kijinsia na mchango wa wanawake katika maendeleo ya taifa.

Mgeni rasmi katika maadhimisho hayo alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, ambaye katika hotuba yake aliwatambua na kuwapongeza wanawake kwa mchango wao mkubwa katika maendeleo ya jamii na taifa kwa ujumla.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mhe. Senyamule alisema kuwa pamoja na kuwepo wanawake wengi mashujaa na wachapakazi nchini Tanzania, taifa lina bahati ya kipekee kuwa na mwanamke jasiri anayeliongoza taifa kwa uthabiti na maono, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan.

Alisema uongozi wa Dkt. Samia umeendelea kuonesha taswira ya wazi ya uwezo, ujasiri na nguvu ya mwanamke katika kusimamia maendeleo ya nchi, hususan kupitia utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo inayogusa maisha ya wananchi moja kwa moja, ikiwemo miradi ya kimkakati ya maji inayotekelezwa katika maeneo mbalimbali ya nchi.

“Mwanamke wa mfano hapimwi kwa vikwazo anavyopitia bali hupimwa kwa namna anavyokabiliana navyo na kuvivuka ili kuleta tabasamu kwa jamii,” alisema Mhe. Senyamule huku akiwahimiza wanawake kuendelea kuwa jasiri na wabunifu katika kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo.

Aidha, alisisitiza kuwa bado kuna wajibu mkubwa kwa jamii na taasisi mbalimbali kuhakikisha wanawake wanapata fursa sawa katika elimu, ajira, uongozi na uchumi ili waweze kufikia malengo yao na kuchangia kikamilifu maendeleo ya taifa.

“Niwajibu wetu kama jamii kuhakikisha ndoto za mtoto wa kike zinatimia. Mafanikio ya mwanamke hayaji kwa urahisi; yanahitaji juhudi, uvumilivu, uthubutu na kutokata tamaa,” aliongeza Mhe. Senyamule.

Kwa upande mwingine, aliwahimiza wanawake wa Mkoa wa Dodoma na Tanzania kwa ujumla kujikita zaidi katika shughuli za kiuchumi na maendeleo, huku wakilinda na kudumisha amani, mshikamano na utulivu wa nchi ambao ni msingi muhimu wa maendeleo endelevu.

Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani kwa Mkoa wa Dodoma mwaka 2026 yamefanyika katika Viwanja vya Wilaya ya Kongwa, yakihusisha wadau mbalimbali kutoka sekta za umma na binafsi, mashirika ya kijamii pamoja na wananchi kwa ujumla.

Maadhimisho hayo yamefanyika chini ya kaulimbiu isemayo: “Haki na Usawa kwa Wanawake na Wasichana: Msingi Jumuishi wa Kufikia Dira ya Maendeleo 2050.” Kaulimbiu hiyo inalenga kuhimiza jamii kuhakikisha wanawake na wasichana wanapata haki na fursa sawa katika nyanja zote za maendeleo ili kufikia jamii jumuishi na yenye usawa.