Habari
Wizara za Maji Zanzibar na Tanzania Bara waahidi kudumisha ushirikiano

Maafisa kutoka Wizara ya Maji, Nishati na Madini Zanzibar wakiongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Mngereza Miraji Mzee wamekamilisha ziara yao ya siku mbili mjini Dodoma huku wakiahidi kuhakikisha ushirikiano wa pande mbili za mungano unadumishwa. Akizunguza mara baada ya ziara hiyo Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Mngereza Miraji Mzee amesema ndoto za waasisi wa Muungano ilikuwa kuhakikisha changamoto za huduma ya majisafi, salama na yenye kutosheleza kwa jamii zinatatuliwa.
“Ndoto za wazee wetu waasisi wa Muungano ilikuwa kuhakikisha tunawezesha maisha bora kwa watu wetu. Sisi kama Wizara inayohusika na Maji, Nishati na Madini tumekuja kujifunza kinachofanyika Tanzania Bara ili kushirikishana mbinu sahihi ya kutatua changamoto zinazazoikumba jamii yetu.”
Amesema changamoto nyingi za huduma ya maji kwa pande mbili zinafanana hivyo kutembeleana na kushirikishana mbinu mbalimbali za utatuzi itasaidia kuharakisha maendeleo.
kwa upande wake Waziri wa Maji upande wa Tanzania Bara. Mhe. Jumaa Aweso. (Mb) amesema Wizara anayoiongoza haitakuwa kikwazo kuhakikisha ushirikiano unadumishwa ili kuwawezesha wananchi wa pande mbili kupata huduma ya Majisafi, salama na yenye kutosheleza.
Ujumbe huo kutoka Zanzibar wametembelea eneo la Mzakwe mjini Dodoma ambalo ni chanzo kikuu cha maji yanayosambazwa mjini Dodoma