Habari

Imewekwa: Nov, 18 2026

​Wizara ya Maji yapongezwa mradi wa maji Kilwa

News Images

Wizara ya Maji imepongezwa kwa jitihada za kutekeleza Mradi wa Maji wa Miji 28 Wilaya ya Kilwa, mkoani Lindi, ambao umefikia asilimia 97.4 ya utekelezaji na tayari umeanza kutoa huduma kwa wananchi, hatua inayotoa matumaini ya upatikanaji wa huduma ya majisafi na salama kwa wakazi wa eneo hilo.

Pongezi hizo zimetolewa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius Ndejembi, wakati wa ziara yake wilayani Kilwa, ambapo ameelekeza Wizara ya Maji kupanua huduma ya mradi huo ili kufikia vijiji jirani vinavyozunguka eneo la mradi.

Agizo Hilo amelitoa kufuatia ombi la Mbunge wa Kilwa Kusini, Mhe. Hasnain Dewj.

Amesisitiza kuwa nia ya serikali ni kuhakikisha huduma ya majisafi inawafikia wananchi wote.

Akizungumza katika ziara hiyo, Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso (Mb), amemhakikishia Makamu wa Rais kuwa Wizara itatekeleza agizo hilo kwa haraka, akieleza kuwa chanzo cha maji cha Mto Mavuji kina uwezo wa kutosheleza mahitaji ya wananchi na mradi umezingatia mahitaji ya huduma ya maji kwa kipindi kirefu.

Mradi huo wenye thamani ya Shilingi bilioni 44.2 unatarajiwa kuhudumia wakazi wapatao 59,983 katika maeneo ya Kilwa Masoko, Kilwa Kivinje pamoja na vijiji vya Mavuji na Mchakama. Utekelezaji wake ni sehemu ya jitihada za Serikali kupitia Wizara ya Maji kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya majisafi na salama, sambamba na kuondoa adha ya upatikanaji wa maji katika maeneo mbalimbali nchini.