Habari

Imewekwa: Dec, 07 2023

Waziri wa Maji awahakikishia wananchi wa Hanang’ huduma ya maji kwa kuchukua hatua za dharura

News Images

Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso (Mb) amesema kufuatia maporomoko na mavuriko kutoka mlima Hanang’, Wizara ya Maji inachukua hatua ya dharura kwa kuweka matanki ya maji ya dharura 30 katika kambi, vituo vya huduma za afya na maeneo yote ya vijiji vilivyoathirika katika kata za Gendahabi, Jorodom, Ganana, Katesh, Mogitu na Dumbeta.

Waziri Aweso akiwa mji wa Katesh amekabidhi kwa madiwani matanki ya maji 30 yenye uwezo wa kubeba lita 5,000 na kusema pamoja na matanki hayo, yatapelekwa magari ya kubeba maji (Maboza) matano yatakayofanya kazi ya kubeba maji kupeleka katika matenki na kufikisha huduma ya majisafi kwa wananchi.

Pamoja na hilo, amekagua mitambo ya kuchimba kisima cha maji ambayo tayari imeanza kazi ili kusaidia kuongeza maji katika vyanzo ambavyo havijaaribiwa na mafuriko. Pia, katika kurejesha huduma ya maji amekabidhi kwa wananchi bomba zenye urefu wa mita 2880.

Miongoni mwa madhara ya mafuriko hayo ni vifo na majeruhi, uharibifu wa mali, na kuharibika kwa miundombinu ya huduma ya maji.

Kitengo cha Mawasiliano