Habari

Imewekwa: Dec, 22 2025

Teknolojia na Tathmini ya Kina Kuimarisha Sekta ya Maji Tanzania

News Images

Wizara ya Maji inaendelea kuboresha huduma kwa wananchi kupitia mapinduzi ya kiteknolojia na tathmini ya kina ya huduma katika Sekta ya Maji, hatua zinazolenga kuondoa malalamiko ya wateja na kuhakikisha upatikanaji endelevu wa maji.

Naibu Waziri wa Maji, Mhe. Mhandisi Kundo Mathew (Mb), amesema matumizi ya teknolojia kama dira za malipo kabla (pre-paid meters) ni mwelekeo wa Serikali. Hatua hii inalenga kuwezesha kila mwananchi kulipia huduma kulingana na matumizi yake, na pia kupunguza malalamiko kuhusu ankara za maji.

Akiongea mkoani Iringa na watumishi wa Sekta ya Maji mkoani humo, Mhandisi Kundo amesisitiza umuhimu wa Mamlaka za Maji kushirikiana na wadau wa maendeleo na Sekta Binafsi ili kuharakisha ufungaji wa dira za malipo kabla. Amesema dira hizo zitasaidia ukusanyaji wa mapato kwa uhakika na kutoa uwazi kwa wateja kuhusu matumizi yao ya maji.

Aidha, Naibu Waziri Kundo amezitaka taasisi zote za Sekta ya Maji mkoani Njombe kufanya tathmini ya kina ya hali ya huduma ya maji na kutoa takwimu sahihi na zinazohitajika. Hii itaiwezesha Wizara kupanga vipaumbele vya utekelezaji wa miradi mipya na kuboresha upatikanaji wa huduma kwa wananchi.

Mhandisi Kundo amesisitiza kuwa kila mfanyakazi katika Sekta ya Maji ana jukumu la kuhakikisha utekelezaji wa majukumu yake kwa ufanisi, huku ushirikiano kati ya taasisi mbalimbali za maji ukiimarishwa na kujifunza kutokana na miradi iliyofanikiwa. Pia, amehimiza umuhimu wa kuwajengea wananchi uaminifu kwa kutoa taarifa muhimu na sahihi zinazohusu huduma ya maji kwa wakati unaofaa, ili kudumisha mahusiano mazuri kati ya Sekta za Maji na jamii.

“Utekelezaji wa dira za malipo kabla na tathmini ya huduma ni hatua muhimu za kuimarisha huduma ya maji, kuhakikisha ukusanyaji wa mapato kwa ufanisi na kutoa huduma bora kwa wananchi wote,” amesema Naibu Waziri Kundo.