Habari

Imewekwa: Dec, 25 2025

Waziri Aweso Atangaza Kutamatika kwa Changamoto ya Maji Dar es Salaam

News Images

Waziri wa Maji, Mheshimiwa Jumaa Aweso (Mb), ameitaka Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) kuhakikisha mitambo yote ya kusukuma maji inawashwa kikamilifu ili kumaliza changamoto ya huduma ya maji kwa wakazi wa Jiji la Dar es Salaam na Mkoa wa Pwani.

Agizo hilo limetolewa kufuatia kuongezeka kwa kiwango cha maji katika Mto Ruvu, hali iliyotokana na utekelezaji wa hatua za dharura katika chanzo cha maji pamoja na kunyesha kwa mvua takribani milimita 50 katika safu za milima ya Uluguru.

Waziri Aweso amesema mgao wa maji kwa wakazi wa Jiji la Dar es Salaam na baadhi ya maeneo ya Mkoa wa Pwani unapaswa kufikia tamati, mara baada ya kutembelea Mtambo wa Maji wa Ruvu Chini uliopo Bagamoyo mkoani Pwani, ambako alishuhudia kurejea kwa mtiririko wa kawaida wa maji katika Mto Ruvu baada ya kipindi cha upungufu wa maji.

Katika hatua nyingine, Waziri Aweso amefafanua kwa kina mipango ya kudumu ya Serikali ya kukabiliana na changamoto ya maji, ikiwemo utekelezaji wa Mradi wa Bwawa la Maji la Kidunda unaotarajiwa kukamilika mwaka 2026.

Aidha, Serikali inaendelea na ujenzi wa awamu ya pili ya Mradi wa Maji wa Visima vya Kigamboni, sambamba na kukamilisha maandalizi ya mpango mkakati wa Mradi wa Maji Rufiji ambao tayari umefanyiwa upembuzi yakinifu.

Kuhusu malalamiko ya wananchi juu ya kubambikiziwa bili za maji licha ya kutopata huduma hiyo, Waziri Aweso ameielekeza DAWASA kufanya uchunguzi wa kina na kuchukua hatua stahiki dhidi ya watakaobainika kuhusika na vitendo hivyo.

Akisisitiza umuhimu wa kuzingatia sheria na haki za wateja, Waziri Aweso amesema kutoa ankara ya maji isiyo halali ni kinyume cha sheria, na ameitaka DAWASA kuhakikisha Mikataba ya Wateja inaheshimiwa wakati wote.