Habari
Waziri Mkuu atoa heko Sekta ya Maji

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa (Mb) ameipongeza Wizara ya Maji kwa kazi kubwa inayofanyika katika utekelezaji wa miradi ya maji nchini.
Mhe. Majaliwa amesema hayo akifungua semina ya waheshimiwa Wabunge kuhusu Sekta ya Maji jijini Dodoma.
Amesema Serikali imeelekezwa katika katika Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kutoa huduma ya maji kwa wananchi hadi katika vitongoji, maeneo ya mijini na vijijini.
Mhe. Majaliwa amesema Serikali imefanya mabadiliko makubwa kwa kuanzisha Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) ambapo kila mkoa unasimamiwa isipokuwa jiji la Dar es salaam.
Amesema wawakilishi wa wananchi ambao ni Wabunge wanao wajibu wa kusema maeneo ambayo hayajafikiwa na huduma hiyo ili kazi zaidi ifanyike ya kuwahudumia wananchi.
Akimkaribisha Waziri Mkuu, Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso (Mb) amesema utekelezaji wa miradi ya maji unategemea upatikanaji wa fedha, na Mhe. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ametekeleza hilo kwa dhati, na kuridhia miradi mikubwa ya kimkakati kujengwa ili wananchi wapate huduma ya majisafi, salama na yenye kutosheleza, haswa kumtua mama ndoo ya maji kichwani.
Kitengo cha Mawasiliano