Habari
Waziri Aweso Awataka Watanzania Kuthamini Rasilimali za Maji

Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso (Mb) amewataka watanzania kutambua umuhimu wa rasilimali za maji kwa kuwajibika kuzitunza na kuzithamini kwa maendeleo ya taifa na mtu mmoja mmoja.
Waziri Aweso ametoa rai hiyo wakati akifungua Mkutano wa 5 wa Jukwaa la Taifa la Wadau wa Sekta Mtambuka katika Usimamizi wa Rasilimali za Maji katika Ukumbi wa Mikutano wa Benki Kuu ya Tanzania, jijini Dar es Salaam.
Akizungumza katika mkutano huo Aweso amesema kuwa thamani ya rasilimali za maji katika uchumi wa nchi yetu ni kubwa kwa sekta zote ikiwemo kilimo, uvuvi, mifugo, nishati, ujenzi, uchukuzi. Hivyo, kuijua thamani ya maji pia itasaidia kubadilisha mtizamo wa wadau na kuweka mikakati ya pamoja ya utunzaji na uendelezaji wa rasilimali za maji.
Waziri Aweso amesema jukwaa hilo lina umuhimu mkubwa katika kuhakikisha usimamizi endelevu wa rasilimali za maji kwa maendeleo ya kizazi cha sasa na baadae. Akitoa rai kuwa jukwaa hilo litumike kutafakari, kujifunza kutoka nchi nyingine na kufanya tathmini ya kina ya kujua thamani ya maji nchi.
Aidha, Waziri Aweso amezindua Programu ya Uongozi wa Maji duniani wenye lengo la kuwahamasisha viongozi wa kisiasa kuhamasisha utunzaji wa rasilimali za maji na Mpango Mkakati wa Jukwaa la Taifa la Wadau Mtambuka wa Rasilimali za Maji unaoainisha muundo na uendeshaji wa jukwaa, vikundi kazi mahsusi pamoja na upatikanaji wa fedha za kuendesha shughuli za jukwaa.
Akisisitiza kuwa mpango mkakati huo uliondaliwa na Wizara ya Maji kwa ushirikiano na Taasisi ya 2030 WRG ulioshirikisha wadau mbalimbali, akisisitiza kuwa mpango uzingatiwe katika uendeshaji wa jukwaa hilo.
Waziri Aweso amezishukuru taasisi za 2030 Water Resources Group na Global Water Partnership (GWP) Tanzania, Ubalozi wa Canada nchini Tanzania pamoja na washirika wengine ambao wameendelea kuchangia kwa hali na mali katika kufanikisha uwepowa jukwaa hili.
Awali akizungumza katika mkutano huo, Balozi wa Canada nchini Tanzania, Mhe. Pamella O’Donell amesema kuwa maji ni msingi wa maendeleo na kichocheo kikubwa katika mafanikio ya Tanzania na umuhimu wa kutunza na kusimamia rasilimali za maji na upatikanaji wa huduma ya majisafi na salama kwa manufaa ya watanzania.
Hivyo, anatarajia kuimarika kwa ushirikiano baina ya sekta binafsi za nchi za Tanzania na Canada katika uwekezaji, teknolojia na kujenga uwezo katika Sekta ya Maji kwa manufaa ya watanzania.
Kaulimbiu ya Mkutano huu wa Jukwaa la Kitaifa la Wadau wa Sekta Mtambuka katika usimamizi wa Rasilimali za Maji ni “Thamani ya maji - Mchango wa Rasilimali za maji kwenye uchumi wa nchi” (Value for Water - Contribution of Water Resources in the Economy of the Country), inayosisitiza umuhimu wa rasilimali za maji kwenye kuchangia uchumi wa nchi.
Mkutano huo ulitanguliwa na vikao vya Kamati ya Uendeshaji ya Jukwaa hilo (Forum Steering Committee) na Vikundi Kazi (Working Groups) vilivyokuwa na malengo ya msingi ya kupitia hadidu za rejea za vikundi kazi hivyo, kuwezesha utekelezaji mzuri wa maamuzi ya jukwaa na namna ya kupima matokeo, pamoja na kuandaa mikakati endelevu ya jukwaa.