Habari

Imewekwa: Dec, 20 2019

Watendaji na wataalam wa Wizara waaswa kushirikiana

News Images

Dodoma; 20 Desemba, 2019

WATENDAJI NA WATAALAM WA WIZARA WAASWA KUSHIRIKIANA

Waziri wa Maji Mhe. Prof. Makame Mbarawa (Mb) amewataka wataalam na watendaji wa Wizara ya Maji kufanya kazi kwa kushirikiana ili kuleta ufanisi katika kufikia malengo ya sekta ya maji nchini.

Prof. Mbarawa amesema hayo wakati akitoa mwelekeo wa sekta ya maji katika Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Huduma za Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira jijini Dodoma.

“Kuna changamoto kubwa ya ukusanyaji mapato katika Mamlaka za Maji nchini, kama wataalam tunatakiwa kufikiria tunaondokana vipi na tatizo hili,” Prof. Mbarawa amesema.

Aidha, Prof. Mbarawa amewaagiza wataalam na wakurugenzi katika mamlaka na taasisi zilizo chini ya Wizara ya Maji kuweka mikakati madhubuti kuhusu utendaji kazi.

Hata hivyo, Prof. Mbarawa amesema moja ya changamoto inayoikabili sekta ya maji ni gharama kubwa za ujenzi kutoka kwa wakandarasi hivyo, amesisitiza wataalam wa serikali kujituma katika kujenga miradi ili kupunguza gharama na kufikisha huduma ya majisafi na salama kwa wananchi.

Prof. Mbarawa ameagiza uwekwe utaratibu wa kutuma fedha za usimamizi katika miradi inayotekelezwa na wataalam wa ndani ili kuwawezesha wahandisi hao kusimamia ipasavyo na kufanya ufuatiliaji wa karibu katika kuhakikisha miradi inajengwa katika kiwango kinachokubalika.

Pamoja na hilo, amewataka Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) kushirikiana kwa karibu na mamlaka zote za maji katika kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi, ubora wa ujenzi wa miradi na kuleta ufanisi katika kufikia lengo la Wizara la kumpatia mwananchi majisafi na salama.

Kitengo cha Mawasiliano Serikalini