Habari

Imewekwa: Feb, 06 2021

Wataalamu wa sekta ya maji watakiwa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

News Images

Mkurugenzi wa Rasilimali za Maji Dkt. George Lugomela akizungumza na wataalamu wa wizara (hawapo pichani) wakati wa kufunga mafunzo ya mabadiliko ya tabianchi yaliyofanyika jijini Mwanza.

Wataalamu wa sekta ya maji kote nchini wametakiwa kukabiliana na changamoto mbalimbali zinzazoikabili sekta hiyo ikiwemo mabadiliko ya tabianchi ili kuwezesha uendelezaji na utunzaji wa rasilimali maji.

Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi wa Rasilimali za Maji kutoka Wizara ya Maji Dkt. George Lugomela wakati akifunga mafunzo ya siku tatu ya wataalamu wa sekta ya maji yaliyofanyika jijini Mwanza.

Amesema dunia inakabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi ambazo kwa kiasi kikubwa zinachangiwa na uvamizi wa shughuli za binadamu kwenye vyanzo vya maji hivyo kupelekea kukauka kwa vyanzo vya maji.

“Jambo linalosikitisha leo ni kwamba hata maeneo ambayo yamebahatika kuwa na vyanzo vya maji, vyanzo hivyo vimepungua uwezo wake wa kuzalisha maji na kupungua kwa ubora wake kutokana na mabadiliko ya tabianchi ambayo yanasababishwa na mambo mbalimbali ikiwemo uchafuzi wa mazingira na uharibifu unaofanywa na wanadamu”.

Amesema Dkt. Lugomela na kusisitiza wataalamu wa sekta ya maji wahakikishe wanakabiliana na mabadilikohayo kwa kushiriki katika utunzaji wa vyanzo vya maji, upangaji sahihi wa ugawaji wa maji na ushiriki wa pamoja katika usimamizi na uendelezaji wa rasilimali za maji.

“Bila kufanya hivyo changamoto ya majisafi na salama itabaki kuwa tatizo lisilotibika kwa nyanja zote za uchumi, afya, teknolojia, siasa, jamii na hata maadili”.

Aidha, Amewaomba washiriki kutumia yale yote waliojifunzakwa ajili ya kuondokana na changamoto zote zinazoweza kuathiri Sekta muhimu za uchumi wa nchi na kusababisha kutofikiwa kwa malengo ya serikali ambayo ni pamoja na kupunguza umasikini.

Mafunzo ya Mabadiliko ya tabia nchi yamehusisha Maafisa kutoka Wizarani, Bonde la Maji la Ziwa Victoria, Bonde la Ziwa Tanganyika na Bonde na yalilenga kutoa nafasi kwa watumishi wa Wizara pamoja na Wadau wengine kutambua umuhimu wa usimamizi wa pamoja wa rasilimali za maji katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.