Habari

Imewekwa: May, 22 2020

Wakandarasi wa Miradi ya Maji Wapewa Onyo Kali

News Images


Naibu Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso (Mb) amewaagiza wakandarasi wote walioitelekeza miradi ya maji kwa sababu ya Ugonjwa wa Virusi vya Corona kurudi kwenye maeneo yao ya kazi kuendelea na utekelezaji haraka.

Naibu Waziri Aweso amekasirishwa na utendaji wa wakandarasi wa Kampuni za M/S Nangai Engineering Ltd na M/S Nipo Africa Engineering Ltd wanaosuasua katika utekelezaji wa ujenzi wa Mradi wa Maji wa Vijiji 6 vya Songambele, Mlowa, Majengo, Tambukareli, Zinginali na Itigi katika Halmashauri ya Itigi, mkoani Singida.

Akisema kuwa zaidi ya Sh. Bilioni 1.3 zimeshatolewa kwenye mradi huo na maendeleo ya kazi yakiwa nyuma ya ratiba na kukwamisha lengo la mradi unaotarajiwa kuhudumia wakazi wapatao 31,000 katika vijiji 6 vinavyozunguka mji wa Itigi unaotegemewa kukamilika ifikapo Mwezi Juni, 2020 kwa gharama za zaidi ya Sh. Bilioni 2.6.

“Nawaagiza wakandarasi wote walioitelekeza miradi ya maji kwa sababu ya Ugonjwa wa Virusi vya Corona warudi kwenye maeneo yao ya kazi na kukamilisha ujenzi wa miradi haraka, ni kweli ugonjwa upo tunachotakiwa ni kuchukua tahadhari lakini kazi zisisimame, atakayekaidi agizo la Serikali tutamchukulia hatua za kisheria kwa kuwa atakuwa anatukwamisha”, ameonya Naibu Waziri Aweso.

Akiwatahadharisha wakandarasi kuacha tabia ya kuitelekeza miradi kwa muda mrefu, na kuonekana kwenye maeneo ya kazi pindi viongozi wa wizara wanapokuwa wakifanya ziara za kukagua miradi hiyo kwa lengo la kuridhisha viongozi hao.

“Watumishi wa Wakala ya Usambazaji Maji na Usafi na Mazingira Vijijini (RUWASA) kazi yenu ni kuwabana wakandarasi wafanye kazi zao usiku na mchana ili miradi isikwame”, Naibu Waziri Aweso amesema.

Mapema Naibu Waziri Aweso alitembelea Mradi wa Maji wa Kintinku-Lisulile katika Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni na kuelekeza mkandarasi alipwe Sh. Milioni 370 anazodai aweze kukamilisha awamu ya kwanza ya ujenzi wa mradi huo, ambapo asilimia 10 imebaki ili awamu hiyo ikamilike.