Habari

Imewekwa: Oct, 10 2020

Vitengo vya Habari Vitumike Kubaini Kero za Jamii katika Sekta ya Maji

News Images

Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Maji Mhandisi Nadhifa Kemikimba amezitaka Bodi za Wakurugenzi za Mamlaka za Maji kuvitumia ipasavyo vitengo vya Habari, Masoko na Huduma kwa Wateja ili kuweza kubaini mahitaji ya jamii na changamoto za kufanyia kazi katika sekta ya maji.

Mhandisi Kemikimba amesema hayo wakati akizindua Bodi ya Wakurugenzi wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Bukoba (BUWASA) tarehe 9 Oktoba 2020 mjini Bukoba. Bodi hiyo mpya ni ya nane katika kuiongoza Mamlaka hiyo na imeelekezwa kuanza na kazi ya kuongeza mtandao wa majisafi na kufikisha huduma hiyo katika maeneo ya viwanda na makazi ya wananchi.

Mhandisi Kemikimba amesema zipo changamoto zinazohusu huduma ya maji katika jamii ambazo lazima zifanyiwe kazi mara moja na sio sawa kusubiri viongozi wa kitaifa au mkoa katika kutafuta utatuzi wake wakati mamlaka za maji zipo.

“Nazitaka mamlaka zote za maji ziwatumie watumishi katika vitengo vya Habari, Masoko na Huduma kwa Wateja kushiriki na kutumia weledi wao kuwasaidia wananchi kufaidi huduma ya majisafi na salama bila kuwa na kero” Mhandisi Kemikimba amesema na kuongeza wataalam wa sekta ya maji wajikite zaidi katika kutoa huduma ya majisafi, salama na yenye kutosheleza jamii.

Ameongeza kuwa lengo la Serikali katika miradi yote ya maji inayotekelezwa nchi nzima ni kutoa huduma bora kabisa ya maji kwa wananchi wote, wanaoishi mijini na vijijini, na ubora wa maji ni jambo la kuzingatia wakati wote kwa afya za wananchi na wateja wa mamlaka za maji.

Mhandisi Kemikimba katika hafla hiyo ya uzinduzi amewaelekeza wataalam wote katika sekta ya maji kutoka Wakala wa Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA), Bodi za Maji za Mabonde na Maabara za Maji kutekeleza kazi kwa pamoja katika kufanikisha huduma bora ya maji kwa Watanzania.

Uzinduzi wa bodi ya BUWASA umehudhuriwa na wadau mbalimbali wa sekta ya maji kutoka serikalini, sekta binafsi, watumishi wa umma waliopo kazini na waliostaafu, viongozi wa mamlaka za Serikali za Mitaa na wawakilishi wa AZAKI.

Kitengo cha Mawasiliano