Habari

Imewekwa: Oct, 25 2025

Kamati ya Usalama Yaridhishwa na Utekelezaji wa Miradi ya Maji Morogoro Mjini

News Images

Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Morogoro, ikiongozwa na Mkuu wa Wilaya Mhe. Mussa Kilakala, imetembelea na kukagua maendeleo ya utekelezaji wa miradi ya maji inayoendelea kutekelezwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Morogoro (MORUWASA) katika maeneo mbalimbali ya Manispaa ya Morogoro, ikiwemo Mkundi, Lukobe, Kiegea, Mindu, Kihonda Mizani na Mkambarani.

Lengo la ziara hiyo lilikuwa ni kujionea hatua zilizofikiwa katika utekelezaji wa miradi hiyo inayolenga kuboresha upatikanaji wa huduma ya majisafi na salama kwa wananchi wa Manispaa ya Morogoro.

Kamati ilionesha kuridhishwa na kasi ya utekelezaji wa miradi na kupongeza juhudi kubwa zinazofanywa na MORUWASA katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora, endelevu na yenye tija baada ya ukaguzi huo.

Akizungumza mara baada ya ziara hiyo, Mhe. Kilakala ameitaka MORUWASA kuendelea kusimamia kwa karibu utekelezaji wa miradi yote ili kuhakikisha inakamilika kwa wakati, kwa viwango vinavyokubalika na kwa manufaa ya wananchi.

“Tunataka kuona miradi hii inakuwa ya mfano na inaleta matokeo chanya kwa wananchi wa Morogoro,” Mhe. Kilakala amesema.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa MORUWASA, Sais Kyejo, amemshukuru Mkuu wa Wilaya na Kamati ya Usalama kwa kufuatilia kwa karibu maendeleo ya miradi hiyo. Aliahidi kuwa maelekezo yote yaliyotolewa yatafanyiwa kazi ili kuendelea kuboresha huduma za maji na kuongeza upatikanaji wa majisafi kwa wananchi wa Manispaa ya Morogoro.

Aidha, katika ziara hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Morogoro amekabidhi vifaa vya kuunganishia huduma ya maji kwa wananchi waliokamilisha taratibu za maombi ya maji katika nyumba zao, hatua inayodhihirisha dhamira ya MORUWASA katika kuhakikisha huduma ya majisafi inawafikia wananchi wengi zaidi.