Habari

Imewekwa: Oct, 25 2025

Bodi ya NJUWASA Kuimarisha Mikakati ya Uhifadhi wa Vyanzo vya Maji

News Images

Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mjini Njombe (NJUWASA) imefanya ziara ya kikazi kukagua utekelezaji wa Mradi wa Maji wa Lugenge pamoja na kutathmini hali ya chanzo cha maji cha Ijunilo, kwa lengo la kujiridhisha na kiwango cha maji katika chanzo hicho.

Kupitia ziara hiyo, Bodi imeibaini kupungua kwa kiwango cha maji katika chanzo cha Ijunilo, hali inayochangiwa na shughuli za kibinadamu ikiwemo kilimo kinachofanyika karibu na chanzo hicho. Shughuli hizo zimeonekana kuhatarisha uendelevu wa huduma ya majisafi kwa wakazi wa Mji wa Njombe.

Kufuatia tathmini hiyo, bodi imeazimia kuweka mikakati madhubuti ya usimaizi na utunzaji wa vyanzo vya maji, ikiwemo kutekeleza miradi ya ufugaji wa nyuki kama njia mbadala ya kujenga uelewa na kuzuia shughuli za kilimo ndani ya maeneo ya hifadhi ya vyanzo vya maji.

Katika hatua nyingine, bodi ilikagua maendeleo ya Mradi wa Maji wa Lugenge unaolenga kuongeza upatikanaji wa huduma ya majisafi kwa wananchi wa Njombe. Kwa sasa, kazi kubwa inayoendelea ni uunganishaji wa bomba kuu kutoka chanzo cha maji kwenda kwenye tenki la maji la Wikichi.

Bodi imeagiza mkandarasi anayetekeleza mradi huo kuhakikisha anakamilisha kazi ya uunganishaji wa mabomba ndani ya siku 14, ili wananchi waanze kunufaika na huduma hiyo muhimu mapema iwezekanavyo.

Aidha, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa NJUWASA, Mhandisi Robert Lupoja amesema mamlaka imepanga kushirikisha wananchi na wadau mbalimbali katika juhudi za kulinda na kuhifadhi vyanzo vya maji, ili kuhakikisha vinabaki salama na endelevu kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.