Habari
Naibu Waziri Kundo Aridhika na Utekelezaji wa Mradi wa Maji wa Kiwira
Naibu Waziri wa Maji, Mhe. Mhandisi Kundo Mathew (Mb), amepongeza kasi na ubora wa utekelezaji wa Mradi wa Maji wa Kiwira unaotumia chanzo cha Mto Kiwira, akisema ni mradi wa kiwango cha juu unaoonesha dhamira ya dhati ya Serikali katika kuboresha huduma ya maji kwa wananchi.
Akikagua mradi huo unaotekelezwa chini ya usimamizi wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mbeya (Mbeya UWSA), Naibu Waziri Kundo amesema Serikali imejipanga kikamilifu kumaliza changamoto ya uhaba wa maji nchini kwa kuwekeza fedha nyingi katika Gridi ya Maji ya Taifa.
Amesema Wizara ya Maji inaendelea kutafsiri maelekezo ya Rais kwa vitendo kupitia usimamizi makini wa miradi ya maji, huku akitoa wito kwa wananchi kushiriki kikamilifu katika kulinda vyanzo vya maji kwa kuepuka shughuli za kibinadamu karibu na vyanzo hivyo ili kuhakikisha upatikanaji endelevu wa rasilimali maji.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Maji Mbeya (Mbeya UWSA), Gilbert Kayange, amesema utekelezaji wa mradi umefikia asilimia 46 na ukikamilika utaongeza uzalishaji wa maji kutoka lita milioni 74 hadi lita milioni 193 kwa siku. Ukitarajiwa kuhudumia Wananchi zaidi ya milioni moja laki tano wa Jiji la Mbeya, Mji wa Mbalizi na Vijiji vinavyopitiwa na mradi.
Mradi huo unagharimu jumla ya shilingi bilioni 119, ambapo hadi Desemba 2025 Serikali imelipa shilingi bilioni 26.4 kwa Mkandarasi na Mhandisi Mshauri. Mradi unahusisha ujenzi wa banio, ulazaji wa bomba kuu lenye kipenyo cha milimita 1,200 kwa umbali wa kilomita 37.24, pamoja na ujenzi wa miundombinu ya kutibu na kuhifadhi maji katika maeneo ya Nsenga na New Forest.
Mradi wa Maji wa Kiwira unatekelezwa kwa mfumo wa usanifu na ujenzi (Design and Build) na Mkandarasi China Railway Construction Engineering Group kwa kushirikiana na China Railway No. 4 Engineering Group, chini ya usimamizi wa Kampuni ya GKW Consultant GmbH.

