Habari

Imewekwa: Aug, 11 2020

Tanzania na Denmark Zaimarisha Ushirikiano Sekta ya Maji

News Images

Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga amekutana na kuzungumza Balozi wa Denmark nchini Tanzania, Mhe. Mette Dissing Spandet kuhusu ushirikiano baina ya nchi hizo kwenye Sekta ya Maji.

Mazungumzo hayo ya awali yalilenga ufadhili wa utekelezaji wa ujenzi wa miradi ya maji hususan kwenye maeneo ya usambazaji wa majisafi na usafi wa mazingira kwenye majiji ya Dodoma na Dar es Salaam, kabla ya kukutana tena na kujadili masuala ya kiufundi katika kutekeleza miradi hiyo.

"Kikao hiki ni cha awali, tumezungumza namna tutakavyotekeleza ujenzi wa miradi katika makao makuu ya Serikali Dodoma na Jiji la Biashara la Dar es Salaam kwa dhumuni la kuhakikisha huduma ya majisafi na majitaka inamairika kwa kuwa ni maeneo yenye mkusanyiko mkubwa wa watu, taasisi nyingi na viwanda vingi na tutakuwa na kikao kingine kwa lengo la kujadiliana masuala ya kiufundi jinsi tutakavyofanya kazi hiyo", amesema Mhandisi Sanga.

Aidha, Balozi wa Denmark, Mhe. Spandet amesema Denmark imekuwa ikifadhili miradi ya maji na imeona mafanikio makubwa kwenye sekta hiyo, akisisitiza itaendelea kutoa fedha kwa Tanzania kupitia Shirika lake la misaada (DANIDA) ili kutimiza lengo la ushirikiano kati nchi hizo mbili.

Kikao hicho kilihusisha wajumbe kutoka Wizara ya Maji, Mkuu wa Masuala ya Ushirikiano katika Ubalozi wa Denmark, Mette Bech pamoja na Msimamizi wa Idara ya Uwekezaji na Biashara katika Ubalozi wa Denmark, Oscar Mkude.