Habari
Naibu Waziri Kundo Atoa Siku 60 Kukamilisha Mtandao wa Mabomba Serengeti
Naibu Waziri wa Maji, Mhe. Mhandisi Kundo Mathew (Mb), ametembelea Mradi wa Maji wa Miji 28 wilayani Serengeti, mkoani Mara na kumuagiza mkandarasi kukamilisha ujenzi wa kilomita 30 za mtandao wa mabomba ndani ya siku 60.
Mhandisi Kundo amesema kuwa hajaridhishwa na kasi ya utekelezaji wa mradi huo ambao awali ulipangwa kukamilika Aprili 2025. Amefafanua kuwa serikali imekuwa ikitoa fedha kwa wakati na haina deni lolote kwa mkandarasi, hali iliyopaswa kuwezesha mradi kukamilika kwa mujibu wa mkataba.
Amebainisha baadhi ya kasoro kwa mkandarasi kuwa ni pamoja na kuwa na idadi ndogo ya wafanyakazi isiyolingana na masharti ya mkataba, baadhi ya wafanyakazi kukosa sifa stahiki, kuchelewesha ununuzi wa vifaa vya ujenzi pamoja na kushindwa kuwalipa wafanyakazi kwa wakati.
Kutokana na hali hiyo, amemuagiza mkandarasi, Kampuni ya Mega Engineering & Infrastructure kuongeza idadi ya wafanyakazi na kuwasilisha orodha ya wafanyakazi wote katika Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Serengeti pamoja na Wizara ya Maji – Makao Makuu, ikiwemo taarifa za malipo yao ya kila mwezi ili kuondoa malalamiko.
Aidha, Naibu Waziri Kundo amesisitiza kuwa ndani ya siku 14 vifaa vyote vinavyohitajika kwa ajili ya utekelezaji wa mradi viwe vimewasili eneo la kazi. Pia amemtaka mkandarasi mkuu kufika ndani ya siku tatu kwa ajili ya kikao cha majadiliano na kupokea maelekezo ya kina.
Mradi wa Maji wa Miji 28 katika Mji wa Serengeti unatekelezwa kwa gharama ya takribani Sh. bilioni 21 na unatarajiwa kuwahudumia wananchi zaidi ya 166,000.

