Habari

Imewekwa: Jan, 08 2026

​Naibu Waziri wa Maji Aweka Jiwe la Msingi Mradi wa Maji Bunda

News Images

Naibu Waziri wa Maji, Mhe. Mhandisi Kundo Mathew (Mb), ameweka jiwe la msingi la Mradi wa Uboreshaji wa Mtandao wa Mabomba wa Mingungani–Kaswaka wilayani Bunda, mkoani Mara, unaolenga kupunguza upotevu wa maji kutoka asilimia 31 hadi asilimia 20 zinazokubalika kimataifa.

Akizungumza katika hafla hiyo Mhandisi Kundo amesema mradi huo, wenye thamani ya shilingi bilioni 1.4, utanufaisha kata zote za mji wa Bunda zenye wakazi wapatao 227,446, hivyo kuboresha upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama kwa wananchi.

Mhandisi Kundo amesema mchango wa Mbunge wa Bunda Mhe. Esther Bulaya umekuwa chachu ya mafanikio yanayoonekana katika sekta ya maji wilayani Bunda, hususan katika jitihada za kupunguza upotevu wa maji na kuboresha huduma kwa wananchi.

Awali, akiwasilisha kero za wananchi, Mhe. Bulaya amesema mradi huo unagusa moja kwa moja kilio chake cha muda mrefu cha kuuondoa mji wa Bunda katika orodha ya maeneo yenye kiwango kikubwa cha upotevu wa maji.

Ameeleza kuwa ana imani kubwa na usimamizi wa Mkurugenzi wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Bunda (BUWASA), Esther Gilyoma, ambaye ameweza kupunguza upotevu wa maji kutoka asilimia 45 hadi asilimia 31 ya sasa.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji Gilyoma amesema utekelezaji wa mradi huo umefikia asilimia 50, na ameishukuru Serikali kwa kuendelea kuwekeza katika Sekta ya Maji wilayani Bunda, akisema kuwa zaidi ya Sh. bilioni 28 zimewekezwa katika miradi mbalimbali ya maji inayoendelea kutekelezwa.