Habari

Imewekwa: Jul, 12 2019

Serikali yasaini Mkataba wa Euro 6.0 milioni na Serikali ya Ujerumani

News Images

Wizara ya Maji kwa niaba ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imetiliana saini Mkataba wa Euro 6.0 milioni na Serikali ya Ujerumani. Mkataba huu ni muendelezo wa Ushirikiano uliopo wa muda mrefu kati ya serikali ya Tanzania na Ujerumani katika kusaidia sekta ya maji nchini.

Akizungumza wakati wa uwekaji saini wa Mkataba huo uliofanyika katika Makao Makuu ya Ofisi za Wizara zilizopo katika Mji wa Serikali Mtumba Katibu Mkuu Wizara ya Maji Profesa Kitila Mkumbo amesema fedha hizo zitatumika katika kuboresha maeneo makuu matatu ambayo ni kuimarisha taasisi zote zinazosimamia rasilimali za maji hasa mabonde kwa kuwanunulia vifaambalimbali vya kuwawezesha kufanya kazi zao vizuri za kupima maji, kuboresha huduma ya maji katika miji ya Mbeya, Tunduma na Ruvuma na pia kujenga uwezo wa taasisi kupitia watalaam mbalimbali waliopo katika sekta ya maji.

Aidha, Katibu Mkuu amewataka watendaji wa Wizara kufanya kazi kwa weledi nakutekeleza majukumu yao ili kuharakisha utendaji wa kazi zote zilizoainishwa katika mkataba.

“Serikali ya awamu hii ni serikali ya kutaka kuona matokeo na si vinginevyo” alisema Profesa Kitila.

Akizungumza kwa niaba ya Serikali ya Ujerumani Mwakilishi wa GIZ Tanzania Dr. Johaness Schoeneberger amesema anategemea kuona matokeo mazuri ya mkataba ambao Serikali ya Ujerumani na Tanzania zimesaini katika kuboresha huduma za sekta ya maji hasa katika kutunza rasilimali za maji hapa nchini.