Habari

Imewekwa: Nov, 10 2021

Serikali Yaimarisha Upatikanaji wa Huduma ya Maji Vijijini

News Images

Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso (Mb) amesema kiwango cha upatikanaji wa huduma ya maji vijijini kimeongezeka kutoka asilimia 64.8 mwaka 2019 hadi asilimia 72.3 kufikia mwezi Juni 2021.

Akisema kuwa hadi sasa, jumla ya vijiji 8,708 kati ya 12,327 vinapata huduma ya maji baada ya kukamilika kwa miradi 1,139 ya maji vijijini chini ya utekelezaji wa Wakala wa Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) wakati akielezea mafanikio ya Sekta ya Maji kwa kipindi cha miaka 60 ya Uhuru wa Tanzania Bara kwa vyombo vya habari, Jijini Dodoma.

Waziri Aweso ameongeza kuwa Serikali kwa kushirikiana na Washirika wa Maendeleo inatekeleza miradi mbalimbali kupitia program za malipo kwa matokeo zinazolenga kuhakikisha uendelevu wa miradi ya maji vijijini na jumla ya Shilingi bilioni 688.81 zimetumika kuboresha huduma ya maji vijijini.

Aidha, amesema kuwa katika mwaka 2021/22, Serikali imepanga kutekeleza miradi 1,176 ya majisafi na usafi wa mazingira vijijini dhumuni likiwa ni kufikisha asilimia 85 ya upatikanaji wa huduma ya maji vijijini ifikapo mwaka 2025.

Waziri Aweso amesisitiza kuwa Wizara ya Maji inaendelea na mikakati ya kuboresha upatikanaji wa huduma ya majisafi na salama kwa wananchi kwa kupanga kutumia Shilingi bilioni 139.4 kutekeleza miradi 218 ya maji nchini kote.