Habari

Imewekwa: Mar, 20 2024

​Serikali inatekeleza miradi ya maji kwa kasi ili kukidhi mahitaji ya wananchi - Prof. Kitila.

News Images

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-Mipango na Uwekezaji Prof. Kitila Mkumbo (Mb) amesema serikali inawekeza katika Sekta ya Maji ili kukidhi mahitaji ya wananchi. Amesema hayo akifungua Mkutano wa Mapitio ya Sekta ya Maji 2024 jijini Dodoma ikiwa ni sehemu ya Maadhimisho ya Wiki ya Maji Kitaifa 2024.

Akiongea kwa niaba ya Waziri wa Maji Mhe. Prof. Kitila amesema lengo kubwa la Serikali ni kukuza uchumi shindani na kuleta maendeleo ya watu na huduma ya maji ni moja ya jambo muhimu katika kufanikisha hatua hiyo hapa nchini.

“Watendaji wa Sekta ya Maji wanafanya kazi kubwa na nzuri, tena usiku na mchana kwa ajili ya wananchi” Mhe. Prof. Kitila amesema na kuongeza Waziri wa Maji halali akipambania masuala ya maji kufika katika makazi ya wananchi.

Amesema hali ya upatikanaji wa maji imezidi kuongezeka mjini na vijijini na kwa kasi ilivyo, malengo yaliyowekwa na serikali yatafikiwaasilimia 85 vijijini na 95 mijini, na kuongeza kuwa takwimu za hali ya upatikanaji wa maji inatokana na uwekezaji unaofanywa na serikali katika kufikisha huduma yam aji kwa wananchi.

Mhe. Prof. Kitila amesisitiza suala la upotevu wa maji (NRW) lifanyiwe kazi zaidi kwa sababu linaongeza gharama za uendeshaji na Wakurugenzi wa Mamlaka za Maji wapimwe katika hatua wanazochukua kuzuia upotevu wa maji.

Pamoja na hayo, amepongeza kazi ya utunzaji na uendelezaji wa vyanzo vya maji hapa nchini hatua ambayo moja ya matunda yake ni kujaa mapema kwa maji katika bwawa la kufua nishati ya umeme la Nyerere, kabla ya muda uliokisiwa ambapo kazi kubwa iliyofanywa na wataalamu wa Sekta ya Maji ni moja ya hatua zilizoitoa Tanzania kimasomaso katika mradi huo mkubwa.

Katika hatua nyingine, Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Maji (NWF) Haji Nandule amekabidhi hundi ya shilingi milioni 800 kwa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Bunda baada ya kuwa mamlaka ya kwanza kukidhi vigezo vya mkopo nafuu unaotolewa kwa ushirikiano na Benki ya Uwekezaji (TIB).

NWF inatoa fedha za utekelezaji wa miradi ya maji hapa nchini na imefungua dirisha la mikopo ya masharti nafuu kwa kushirikiana na Benki ya TIB hatua ambayo inafanikisha huduma ya miradi ya maji kwa jamii kupitia mamlaka za maji.

Kitengo cha Mawasiliano