Habari

Imewekwa: Mar, 19 2026

Serikali yajidhatiti kutoa huduma bora kwa wananchi

News Images

Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso (Mb), amesema Serikali imejidhatiti kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za majisafi na usafi wa mazingira kwa mageuzi ya sekta na usimamizi madhubuti wa mamlaka za maji nchini.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa Taarifa ya Utendaji wa Mamlaka za Majisafi na Usafi wa Mazingira kwa Mwaka 2024/25, Waziri Aweso amesisitiza kuwa tathmini iliyofanywa na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) inapaswa kutumika kama nyenzo ya kufanya mabadiliko ya kweli katika sekta na kuona Wizara ya Maji inakuwa mfano wa kuigwa kwa sekta nyingine ndani na nje ya nchi.

Amebainisha kuwa pamoja na tathmini ya utendaji, kuna umuhimu mkubwa wa kuwajengea uwezo watendaji wa Sekta ya Maji ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi na kuleta matokeo chanya. Amesisitiza kuwa Bodi za Wakurugenzi za Mamlaka za Maji zinapaswa kuimarishwa ili ziweze kusimamia taasisi hizo na kuhakikisha zinafikia malengo yaliyokusudiwa.

Katika uwajibikaji, Waziri Aweso amesema kuwa utendaji wa Wakurugenzi Watendaji wa Mamlaka za Maji utapimwa kwa kigezo cha namna wanavyokabiliana na changamoto ya upotevu wa maji. “Ni lazima tutatue changamoto ya upotevu wa maji, hili ni eneo muhimu katika kuboresha ufanisi wa huduma za maji nchini, hii ni fedha”, Aweso amesisitiza.

Waziri Aweso amehimiza matumizi ya teknolojia za kisasa katika kushughulikia changamoto mbalimbali za sekta, ikiwemo upotevu wa maji, malalamiko ya ankara za maji, pamoja na ulinzi wa miundombinu na vyanzo vya maji. Pia amesisitiza umuhimu wa kuweka mfumo rasmi wa kisheria utakaowezesha ushirikiano na uwekezaji wa Sekta Binafsi katika Sekta ya Maji ili kuongeza ufanisi na rasilimali fedha.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mhandisi Mwajuma Waziri, amesema utekelezaji wa maelekezo ya Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan unahitaji kutafsiriwa kwa vitendo kupitia utendaji bora wa mamlaka za maji. Ameeleza kuwa maji ni nguzo ya msingi kwa maendeleo ya uchumi na ustawi wa jamii, hivyo mamlaka zinapaswa kuhakikisha upatikanaji wa huduma endelevu na bora kwa wateja.

Awali, Mtendaji Mkuu wa EWURA, Dkt. James Andilile amesema pamoja na mamlaka za maji kuendelea kuimarika, zina kazi kubwa ya kufanya kuimarisha huduma ya upatikanaji wa majisafi na usafi wa mazingira. Amesisitiza uwajibikaji kwa Wakurugenzi Watendaji wa Mamlaka hizo katika kusimamia vizuri rasimali watu, rasilimali fedha pamoja na utekelezaji wa mipango ya taasisi kila mwaka.

Tathmini ya utendaji wa mamlaka umeendelea kuonesha dhamira ya Serikali ya kuhakikisha Mamlaka zote za Maji zinatoa huduma bora kwa wananchi kwa kuzingatia ufanisi, uwajibikaji na matumizi ya rasilimali zake kwa tija. Serikali inalenga kuona mafanikio ya Sekta ya Maji yanapimwa kwa namna yanavyogusa maisha ya wananchi kupitia huduma bora, salama na endelevu.