Habari
Kamati ya Bunge Yapongeza Utekelezaji wa Mradi wa Bwawa la Kidunda
Kamati ya Bunge ya Maji na Mazingira imetoa pongezi kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuidhinisha Shilingi bilioni 335 na kuwezesha utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa Bwawa la Kidunda, mkoani Morogoro.
Kamati hiyo, ikiongozwa na Mwenyekiti wake, Mhe. Jackson Kiswaga (Mb), imebainisha hii hatua baada ya kufanya ziara ya kikazi, ikikagua maendeleo ya ujenzi wa mradi huu muhimu wa bwawa.
“Tunajivunia mradi huu ambao tunatekeleza kwa fedha za Watanzania wenyewe. Huu mradi unalenga kuleta uhakika wa huduma ya maji kwa wakazi wa Dar es Salaam na Pwani, hasa wakati tunakabiliana na ukame na mabadiliko ya tabianchi,” Kiswaga ameeleza.
Kiswaga amefafanua kwamba Kamati ya Bunge ya Maji na Mazingira itaendelea kuishauri Serikali ili kuhakikisha fedha za utekelezaji wa mradi huu hazikwami na kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati, ukiwa na faida za moja kwa moja kwa wananchi.
“Tunashirikiana na Serikali kuhakikisha mradi unatekelezwa kikamilifu, lakini pia tunawaomba wananchi kuendelea kutunza vyanzo vya maji. Uchafuzi wa vyanzo unaleta ujaaji wa tope kwenye bwawa na kupunguza maisha yake, hali ambayo inaweza kusababisha hasara kubwa,” Kiswaga ametoa rai.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Rose Ambrose, amesema Wizara inaendelea kusimamia mradi huu kwa karibu, ikitatua vikwazo vyote vinavyojitokeza ili mradi ukamilike kwa wakati na kuleta tija kubwa kwa wananchi.

