Habari

Imewekwa: Mar, 22 2024

Sekta mtambuka zatakiwa kushirikiana kulinda vyanzo vya maji

News Images

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Dotto Biteko (Mb) ameelekeza Sekta Mtambuka kushirikiana katika kulinda vyanzo vya maji.

Mhe. Dkt. Biteko ametoa agizo hilo wakati wa Siku ya Maji Duniani 2024 iliyofanyika, Mtumba jijini Dodoma.

Amesema Serikali ya Awamu ya Sita imefanya mabadiliko makubwa katika Sekta ya Maji ya ‘kumtua mama ndoo ya maji kichwani’ na Wizara ya Maji imefanikiwa kuongeza upatikanaji wa huduma ya maji mijini na vijijijni

"Niwapongeze kwa kiasi kikubwa kwa jitihada mnazozifanya ya kuongeza upatikanaji wa huduma ya maji kwa wananchi katika sehemu mbalimbali hapa nchini," Mhe. Biteko amesema na kuongeza tunapoadhimisha Siku ya Maji Duniani na wiki ya maji 2024 tujiulize tumewekeza nguvu gani katika kuhifadhi na kulinda vyanzo vya maji kwa maana ni jukumu letu sisi sote ili vizazi vijavyo viweze kunufaika.

Siku ya Maji Duniani imebeba kaulimbiu isemayo "Uhakika wa maji kwa amani na utulivu", na ilitanguliwa na wiki yam aji iliyoshehenu kazi mbalimbali zinazohusu huduma yam aji katika jamii.

Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso (Mb) amesema kuwa mafanikio katika Sekta ya Maji ni matokeo ya kazi kubwa aliyoifanya Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan ambapo amefanikiwa kutoa majibu kwa wananchi kwa miradi iliyokwama kwa muda mrefu tangu mwaka 1970, na kuifanikisha ndani ya kipindi cha miaka mitatu.

"Tunampongeza Mhe. Rais Samia amekuwa na sisi kila muda kuhakikisha tunafanya kazi kubwa na nzuri ya kuongeza upatikanaji wa huduma ya maji kwa wananchi, na sasa tuna vijiji 9737 vinapata huduma ya maji, na vingine 2581 tunamalizia kwa mitambo ya kisasa aliyotununulia" Mhe. Aweso amesema

Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji Mhandisi Mwajuma Waziri katika hafla hiyo amesema Serikali imetambua jitihada za wanawake katika Sekta ya Maji na kwa kuongozwa na Naibu Waziri wa Maji Mhe. Mhandisi Maryprisca Mahundi kazi kubwa ya kuhakikisha maeneo ambayo hakuna huduma ya maji kazi ya kuchimba visima imefanyika katika maeneo mbalimbali ikiwamo Urambo, Kasulu, Kibondo, Iringa, na Misugusugu.

“Lengo la wizara ni kufikisha asilimia 85 vijijini na asilimia 95 mijini kuhusu upatikanaji wa huduma ya maji” Mhandisi Mwajuma amesema

Siku ya Maji Duniani hutanguliwa na Wiki ya maji kila Machi tarehe 16 hadi 22.

Kitengo cha Mawasiliano