Habari
RUWASA yapewa Kongole kwa Kuwafungia wananchi Dira za malipo Kabla

Bodi ya Wakurugenzi wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) wameridhishwa na mageuzi yanayofanywa na wakala hiyo katika matumizi ya Dira za Malipo kabla kwa wateja.
Pongezi hizo zimetolewa na timu ya kamati tatu za RUWASA zilizotembelea mkoa wa Arusha na Kilimanjaro kukagua hatua iliyofikiwa katika matengenezo na matumizi ya Dira za malipo kabla.
Kamati hizo ni Kamati ya Fedha na Utawala, Kamati ya Miradi na Ufundi pamoja na Kamati ya Ukaguzi na Viashiria Hatarishi.
Mwenyekiti wa Kamati ya Fedha na Utawala Profesa Aloys Mvuma amesema mafanikio makubwa yaliyopatikana baada ya majaribio ya awali ya matumizi ya dira hizo yanaashiria kuwa Tanzania inaingia katika mabadiliko makubwa ambayo yatawezesha kuondokana na changamoto nyingi za utoaji wa huduma ya maji kwa wananchi na amewataka wabunifu hao kuendelea kutatua changamoto nyingine ili kuongeza ufanisi.
Awali akiwasilisha hatua iliyofikiwa katika matengenezo ya Dira hizo Mwenyekiti wa Kamati ya Ufundi wabunifu wa Dira hizo kutoka chuo cha Ufundi cha Arusha ambao ni moja ya taasisi zilizopewa jukumu la kubuni na kutengeneza Dira hizo Mhandisi Crecent Sembuli amesema wako katika hatua ya Nne ya maboresho katika kazi hiyo na kwamba hatua zilizochukuliwa zimewezesha kutatua changamoto nyingi zilizoripotiwa katika majaribio ya awali, sasa Dira hizo zinaufanisi mkubwa.
Mwenyekiti wa Jumuia ya watumia maji ya Lawate Fuka wilayani Siha, Nicoloaus Kombe amesema kwa sasa wana uwezo mkubwa wa kupata taarifa muhimu za mapato na matumizi ya fedha baada ya kuanza kutumia Dira hizo tofauti na awali walipokuwa wakitumia Dira za malipo baada ya matumizi.
Ameiomba Wizara ya Maji kusambaza Dira hizo ili matumizi yake yawafikie wananchi katika maeneo mbalimbali nchini.