Habari
Wizara Inahitaji Watumishi Wenye Nia ya Matokeo
Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso (Mb), amesema kuwa Wizara ya Maji inahitaji watumishi wanaofanya kazi kwa bidii, uwajibikaji na nia ya dhati ya kuleta matokeo chanya ili kuimarisha utoaji wa huduma bora ya maji kwa wananchi.
Waziri Aweso ameyasema hayo wakati wa Mkutano wa Mwaka wa Wakala wa Majisafi na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) pamoja na vyombo vya Watoaji wa Huduma ya Maji ngazi ya Jamii (CBWSOs) uliofanyika katika Ukumbi wa Jiji la Dodoma, Mtumba.
Akizungumza katika mkutano huo, Waziri Aweso amesisitiza umuhimu wa mchango mkubwa unaotolewa na CBWSOs katika kusimamia na kuboresha huduma za maji katika jamii. Amesema jumuiya hizo zinatambulika kisheria nchini na zina jukumu muhimu la kuhakikisha huduma ya maji inawafikia wananchi, hususan katika maeneo ambayo hapo awali yalikuwa na changamoto katika upatikanaji wa huduma hiyo.
Aidha, amewataka wadau hao kuendelea kuimarisha usimamizi wa huduma za maji, kuongeza uwajibikaji pamoja na kushiriki kikamilifu katika juhudi za utunzaji wa mazingira ili kuhakikisha vyanzo vya maji vinaendelea kulindwa na kudumishwa.
Katika kusisitiza uwajibikaji kazini, Waziri Aweso amesema Wizara ya Maji haitavumilia wala kuendelea kulea watumishi wazembe wasio na dhamira ya kufanya kazi kwa ufanisi na kuleta matokeo yanayoonekana kwa wananchi.
Amesisitiza kuwa hatosita kuchukua hatua stahiki dhidi ya watumishi watakaobainika kuwa wazembe, ili kuhakikisha lengo la Serikali la kutoa huduma bora, endelevu na kwa wakati kwa wananchi linafikiwa.

