Habari

Imewekwa: Feb, 26 2026

Dkt. Nchemba Apongeza Utekelezaji wa Mradi wa Miji 28 Tanga

News Images

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba (Mb.), ameonesha kuridhishwa na kupongeza utekelezaji wa Mradi wa Maji wa Miji 28 mkoani Tanga, wenye thamani ya takribani Shilingi bilioni 186, wakati wa ziara yake ya kikazi katika Wilaya ya Korogwe, Mkoa wa Tanga.

Akizungumza baada ya kukagua mradi huo unaosimamiwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira ya Handeni Trunk Main (HTM), Dkt. Nchemba alisema Serikali imejipanga kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya majisafi na salama kama ilivyoahidi.

“Serikali ya Awamu ya Sita imeweka kipaumbele kikubwa katika Sekta ya Maji. Mradi huu ni mfano wa kazi kubwa inayofanywa na Serikali kote nchini. Tumewekeza zaidi ya Shilingi bilioni 186 mkoani Tanga kwa ajili ya mradi huu,” alisema Dkt. Nchemba.

Aliongeza kuwa Serikali imefanya uwekezaji mkubwa katika miradi ya maji nchini kote kwa lengo la kumaliza changamoto za huduma ya maji kwa Watanzania wote.

Dkt. Nchemba alibainisha kuwa miradi mikubwa kama Mradi wa Maji wa Miji 28 ni miongoni mwa miradi ya kimkakati ambayo Serikali imejipanga kuitekeleza ili kuleta manufaa kwa taifa.

“Tunataka uwekezaji mkubwa unaofanywa na Serikali katika miradi ya maji utoe manufaa makubwa kwa wananchi na taifa kwa ujumla,” alisisitiza.

Kwa upande wake, Waziri wa Maji, Mheshimiwa Jumaa Aweso (Mb.), alisema kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameielekeza Wizara ya Maji kutumia rasilimali nyingi za maji zilizopo nchini ili kumaliza changamoto za maji zinazowakabili Watanzania.

Alisema Wizara inaendelea kutekeleza Mkakati wa Gridi ya Taifa ya Maji (National Water Grid Strategy) na kubainisha kuwa Tanzania kwa sasa ina jumla ya mita za ujazo bilioni 126 za rasilimali za maji, ambazo zitatumika ipasavyo kwa manufaa ya wananchi.

Awali akiwasilisha taarifa ya mradi huo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mhandisi Mwajuma Waziri, alisema Mradi wa Maji wa Miji 28 unachukua maji kutoka Mto Pangani na umebuniwa kuhudumia Wilaya za Handeni, Korogwe, Muheza na Pangani, pamoja na vijiji 161 vinavyozunguka maeneo hayo.

Mradi huo kwa sasa umefikia asilimia 76 ya utekelezaji. Utakapokamilika, unatarajiwa kuzalisha lita milioni 51 za maji yaliyotibiwa kwa siku na kunufaisha moja kwa moja zaidi ya wakazi 868,000 katika maeneo lengwa.

Mradi wa Maji wa Miji 28 ni sehemu muhimu ya Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji inayotekelezwa na Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo. Ni miongoni mwa uwekezaji mkubwa unaoendelea unaolenga kupanua upatikanaji wa huduma za majisafi na salama nchini kote.