Habari
Rais Samia Aridhishwa na Utekelezaji wa Mradi wa Maji Jiji la Arusha

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ameridhika na maendeleo ya utekelezaji wa mradi wa maji wenye thamani ya Sh. bilioni 520 unaotekelezwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Arusha (AUWSA) katika Jiji la Arusha na kusisitiza kukamilika kwa wakati.
Amesema mradi huo utamaliza changamoto ya upatikanaji wa huduma ya majisafi na salama, pamoja na usafi wa mazingira katika Jiji la Arusha ambalo limekuwa na changamoto ya maji kwa muda mrefu.
Rais Samia amesema hayo baada ya kukagua moja ya vituo vya kusukuma maji vya mradi huo kilichopo katika eneo la Chekereni katika Wilaya ya Arumeru, mkoani Arusha.
“Mradi umeshaanza kutoa huduma kwenye baadhi ya maeneo na kufikia mwezi Juni, 2022 wananchi wote wa Arusha watakuwa wakipata majisafi na salama”, amesema Rais Samia.
Awali, Waziri wa Maji, Mhe. Juma Aweso (Mb) amesema kwa sasa asilimia 63.45 ya wakazi wa Jiji la Arusha wanapata huduma ya majisafi na salama na wakazi 4,000 wananufaika na huduma ya majitaka.
Waziri Aweso amesisitiza kuwa huduma itafika mpaka maeneo ya vijijini kwa kuwa mradi huo ni mkubwa na uzalishaji wake ni lita milioni 200 za maji kwa siku wakati mahitaji ya maji ya Jiji la Arusha ni lita milioni 109 kwa siku.
Mradi huu umefikia asilima 75 kwa sasa, unatarajiwa kukamilika ifikapo mwezi Juni, 2022 ambapo utaongeza uzalishaji wa maji kutoka wastani wa lita 40,000,000 hadi lita 200,000,000 kwa siku na utawezesha utoaji wa huduma ya majisafi kufikia zaidi ya asilimia 100.