Habari

Imewekwa: Feb, 01 2021

RAIS MAGUFULI AZINDUA MIRADI YA MAJI SHINYANGA NA TABORA

News Images

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli amezindua miradi miwili mikubwa ya Maji kutoka Ziwa Victoria.

Mradi wa kwanza unapeleka maji katika miji midogo ya Kagongwa na Isaka Mkoani Shinyanga na mradi wa pili unapeleka maji katika miji ya Tabora, Igunga na Nzega Mkoani Tabora.

Akizindua mradi wa Isaka-Kagongwa Mhe. Rais ameagiza Wizara ya Maji kuhakikisha inasambaza maji kwa wananchi wa kijiji cha Isagehe kuliko jengwa matenki yanayosambaza maji kwenye mji wa Kagongwa. Aidha ihakikishe inatoa huduma ya majisafi na salama kila eneo kunakowekwa miundombinu ya miradi.

Kwa upande wa mradi wa Tabora-Igunga-Nzega ameagiza kupanua mradi ili maji hayo yawafikie wananchi wa miji ya Sikonge, Kaliua na Urambo.

Mhe. Rais ameipongeza Wizara ya Maji kwa kusimamia vizuri utekelezaji wa mradi na ameitaka iendelee na jitihada hizo nzuri.

“Niwapongeze Wizara ya Maji. Kwa mwendo huu naona sasa mnakwenda vizuri," alisema na kuongeza kuwa miradi mingi ya maji ilikuwa haikamiliki kwa wakati.

"Sasa naona mmeanza kuwa na muelekeo mzuri. Waziri, Katibu Mkuu na Watendaji wote endeleeni hivyo.” Alisema Mhe. Rais huku akishangiliwa na Wananchi.

Kwa upande wake Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso (MB) amesema amepokea maagizo ya Mhe. Rais na amewaagiza wataalam wa Wizara yake kuanza utekelezaji mara moja.

Amesema Wizara ya Maji siyo Wizara ya ukame hivyo atahakikisha huduma ya majisafi, salama na yenye kutosheleza yanamfikia kila Mtanzania.

Mradi wa maji wa Isaka-Kagongwa umetekelezwa kwa gharama ya shilingi Bilioni 23.1 fedha za ndani na ule wa Tabora Igunga- Nzega umetekelezwa kwa gharama ya shilingi Bilioni 617.