Habari

Imewekwa: Sep, 11 2025

Watumishi Wenye Sifa Waingizwe Kwenye Mfumo Wa E-Utumishi

News Images

Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Juma Mkomi, amezitaka Mamlaka za Majisafi na Usafi wa Mazingira pamoja na maafisa rasilimali watu kuhakikisha watumishi wote wenye sifa wanaingizwa kwenye mfumo wa E-Utumishi, huku changamoto zozote zinazojitokeza zikitatuliwa kwa wakati.

Mkomi ametoa maelekezo hayo jijini Dodoma wakati wa uzinduzi wa kikao kazi cha siku nne kinachowakutanisha Wakurugenzi Watendaji, Wakurugenzi wa Rasilimaliwatu na Maafisa Rasilimaliwatu wa Mamlaka za Maji nchini, kilichofanyika katika ukumbi wa Makao ya Wizara ya Maji, jijini Dodoma.

Amesema kuwa ni wajibu wa viongozi wa taasisi hizo kufanya tathmini ya mahitaji ya watumishi kupitia mfumo wa Tathmini ya Rasilimaliwatu ili kubaini upungufu uliopo na kujua watumishi wanaohitajika.

“Ni muhimu kuzingatia sera za utumishi na taratibu za ajira zinazoratibu utaratibu wa ajira ili kuhakikisha kila mtumishi anatendewa haki katika utumishi wa umma,” alisema Mkomi.

Aidha, amewataka Wakurugenzi wa Idara na Maafisa Rasilimaliwatu kutojenga vikwazo kwa watumishi bali wawe daraja la kusikiliza na kushughulikia masuala yao.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mhandisi Mwajuma Waziri, amesema Wizara inaendelea kusogeza huduma ya maji kwa wananchi kupitia taasisi zake, na utekelezaji wa jukumu hilo unahitaji rasilimaliwatu wenye weledi na nidhamu ya kazi.

Kikao kazi hicho kimelenga kutoa mafunzo ya matumizi bora ya mifumo ya kiutumishi na kiutawala kwa ajili ya kuboresha huduma katika taasisi za umma.