Habari
Mkurugenzi Mtendaji BUWASA Aridhishwa na Maendeleo ya Mradi wa Maji Nyamuswa

Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Bunda (BUWASA), Esther Gilyoma,ameridhishwa na maendeleo ya utekelezaji wa Mradi wa Maji wa Nyamuswa, baada ya kufanya ziara ya ukaguzi wa mradi huo wa maji unaolenga kuboresha upatikanaji wa majisafi na salama kwa wananchi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bunda.
Mkurugenzi Gilyoma amesema kuwa hadi sasa, mradi umefikia asilimia 26 ya utekelezaji, huku kazi mbalimbali zikiendelea vizuri. “Kazi za uchimbaji wa mtaro wenye urefu wa kilomita 33, ulazaji wa mabomba na vipuri vyake, ununuzi wa bomba, ujenzi wa matangi ya maji, nyumba za watumishi na nyumba za mitambo zinaendelea vizuri. Hii ni ishara tosha kwamba mradi utakamilika kwa wakati na kuleta manufaa makubwa kwa wananchi wa vijiji vyote vinavyonufaika,” Gilyoma amesema.
Mradi wa Nyamuswa unatarajiwa kuwahudumia wakazi wa vijiji vya Bukama, Makongoro A na B, Nyamuswa na Tiring’ati, huku ukilenga kuhakikisha wananchi wanapata majisafi na salama karibu na makazi yao, jambo litakaloondoa changamoto za upatikanaji wa maji ambazo zimekuwa kero kwa kaya nyingi.
Mradi huo wenye thamani ya zaidi ya Shilingi bilioni 8.3 unahusisha ujenzi wa tenki la maji lenye ujazo wa lita 300,000, tenki la chini lenye ujazo wa lita 200,000, pamoja na usakinishaji wa pampu mbili za kisasa za kusukumia maji hadi kwenye matangi yaliyopo Bukama na Makongoro. Aidha, ujenzi wa nyumba za mitambo na makazi ya wahudumu wa mitambo umejumuishwa katika mradi huu, kuhakikisha operesheni za maji zinafanyika bila kasoro.
Baadhi ya wananchi waliokutana na Mkurungenzi Gilyoma mara baada ya ziara hiyo wamefurahia maendeleo ya mradi na kuonesha kuridhishwa na hatua zilizofikiwa hadi sasa, huku wakitarajia kunufaika na huduma ya majisafi na salama mara mradi utakapokamilika.
Pamoja na kuridhishwa na maendeleo ya mradi, Mkurugenzi Gilyoma amemtaka mkandarasi kuongeza kasi ya kazi ili mradi ukamilike kwa wakati na kuanza kutoa huduma kwa wananchi hata kabla ya kukamilika kwa kazi zote kwa asilimia 100.
Gilyoma aliendelea kusisitiza kuwa mradi huu ni sehemu ya jitihada za Serikali za kuboresha huduma za majisafi na usafi wa mazingira katika Halmashauri ya Wilaya ya Bunda, na amewataka wananchi kushirikiana kwa kulinda na kudumisha mradi huu muhimu, ili uwe endelevu na kutoa huduma kama inavyotarajiwa.
“Ushirikiano wa wananchi ni muhimu ili kuhakikisha mradi huu unaleta matokeo chanya. Kwa pamoja tunaweza kuhakikisha upatikanaji wa majisafi na salama unakuwa endelevu na kunufaisha kila kijiji,” Gilyoma ametoa rai.
Mradi huu ulianza rasmi tarehe 1 Februari 2025, unatekelezwa kwa fedha za Serikali na unahusisha wakandarasi Moli Oil Mills kwa kushirikiana na GAT Engineering Co. Ltd.