Habari

Imewekwa: Sep, 10 2019

Profesa Mkumbo Aitaka RUWASA Kufikikisha Huduma ya Maji kwa Wananchi

News Images

TAARIFA KWA UMMA

Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Profesa Kitila Mkumbo amewataka watendaji wa Wakala wa Majisafi na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) kufanya kazi kwa nidhamu, uadilifu na weledi ili kuwapatia wananchi wa vijijini majisafi na salama.

Profesa Kitila amesema kuwa, taasisi yoyote mpya ni lazima ianze kwa kuonesha jamii mwelekeo wake, hivyo ni muhimu taasisi hiyo iwe na watu wenye nidhamu, wawe na nidhamu ya fikra pamoja na nidhamu ya kiutandaji.

Profesa Kitila amesema kuwa, Wizara ya Maji imetimiza wajibu wake wa kuanzisha mchakato wa RUWASA mpaka kuanza kazi zake, sasa ni wajibu wa RUWASA kuhakikisha wanafanya kazi zao na kujibu kero na matatizo ya maji vijijini kwa haraka.

Pia amewataka watendaji wa RUWASA kufanya kazi kwa ufanisi kwa kuzingatia kuwa, wao ni viongozi, watawala na wana weledi katika maeneo yao ya kazi.

Wakati akimkaribisha Katibu Mkuu, Mkurugenzi Mkuu wa RUWASA Mhandisi Clement Kivegalo amesema kuwa, taswira ya wahandisi wa maji nchini siyo nzuri ambayo imetokana na changamoto zilizokuwepo hapo nyuma.

Amesema kuwa, yeye na timu yake wamejipanga vizuri kuhakikisha kuwa kero na matatizo ya maji vijijini yanapatiwa majibu na miradi ya maji vijijini inatekelezwa kwa uhalisia wa thamani ya fedha.

Kitengo cha Mawasiliano

06 Septemba, 2019