Habari

Imewekwa: Jun, 18 2020

Prof. Kitila Mkumbo azindua maabara bora ya uchunguzi wa rasilimali za maji (Isotope Hydrology)

News Images

Katibu Mkuu, Wizara ya Maji, Prof. Kitila Mkumbo amezindua Maabara bora ya Afrika Mashairiki na Kati ya Uchunguzi wa Rasilimali za Maji (Isotope Hydrology) ambayo itasaidia kuboresha usimamizi wa rasilimali za maji nchini.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa maabara hiyo jijini Dodoma, Prof. Mkumbo amesema maabara hiyo ni ya kisasa na imeigharimu serikali fedha nyingi kiasi cha Dola za Kimarekani milioni 62 inakadiriwa kuwa sawa na shilingi milioni 150 za Kitanzania.

Prof. Mkumbo amewaagiza wataalam wa Wizara kuitumia maabara hiyo na vifaa vyake kwa uangalifu ili iweze kutumika kwa muda mrefu na kuboresha usimamizi wa rasilimali za maji na hatimaye kuweza kutoa huduma bora kwa wananchi.

Aidha, Naibu Katibu Mkuu, Mhandisi Anthony Sanga ametoa wito kwa taasisi za elimu hususan kwa wanafunzi wa shule za Sekondari na Vyuo wanaosoma masomo ya Kemia kuja kujifunza kwa vitendo kupitia maabara hiyo na kuona mambo mazuri yanayofanyika Wizara ya Maji.

Akielezea historia ya matumizi ya teknolojia ya Isotope hapa nchini Mkurugenzi wa Rasilimali za Maji Dkt. George Lugomela, alisema yalianzishwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Nguvu za Atomiki kupitia mtaalam mwelekezi Bw. Turgut Dincer kupitia mradi wa ushirikiano wa kiufundi (TC) Project URT/8/003 mwaka 1979.

Dkt. Lugomela alisema Teknolojia ya nguvu za Atomiki hutumika katika nyanja mbalimbali ikiwemo utengenezaji wa silaha, uzalishaji umeme, huduma za afya kwa maana vifaa na tiba ya mionzi pamoja na kuwezesha usimamizi endelevu wa rasilimali za maji kupitia matumizi ya Teknolojia ya Isotope.