Habari

Imewekwa: Aug, 22 2019

Naibu Waziri Aweso Aridhishwa na Utekelezaji wa Mradi Mkubwa wa Maji Arusha

News Images

TAARIFA KWA UMMA

Naibu Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso (Mb) ameridhishwa na maendeleo ya ujenzi wa mradi mkubwa wa maji jijini Arusha na kumtaka mkandarasi aendelee na kasi hiyo aweze kukamilisha mradi huo mapema iwezekanavyo.

Naibu Waziri Aweso amekagua mradi huo wa kimkakati katika Jiji la Arusha na kuridhishwa na kasi ya utekelezaji wa mradi huo na hatua iliyofikiwa mpaka sasa.

Ameeleza kuwa Serikali imewekeza Shilingi bilioni 520 katika Jiji la Arusha ili kuondoa kero ya upungufu wa majisafi na uondoaji wa majitaka katika Jiji la Arusha na baadhi ya maeneo ya Arumeru ili kuendana na kasi ya ukuaji wa Jiji la Arusha.

Mhe. Aweso ametoa pongezi kwa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira jijini Arusha (AUWSA) ambao ni wasimamizi wa mradi na Mkandarasi wa Kampuni ya Sinohydro Corporation Ltd ya China inayotekeleza mradi huo kwa kiwango kizuri cha kazi kilichofikiwa na kutoa matumaini makubwa kwa wakazi wa Arusha na maeneo ya jirani.

Lakini pia, akamtaka mkandarasi kukamilisha ujenzi wa tenki la maji lenye ukubwa wa lita milioni kumi lililopo Seed Farm, Ngaramtoni ifikapo mwezi kumi na maji yaanze kujazwa ifikapo mwezi wa kumi na mbili mwaka huu katika tenki hilo linalojengwa katika Wilaya ya Arusha.

Akisema mradi huo ni moja ya miradi mikubwa itakayoleta mabadiliko makubwa kwenye Sekta ya Maji nchini.

Akitolea ufafanuzi juu ya utekelezaji wa mradi, Mkurugenzi wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira jijini Arusha (AUWSA), Mhandisi Ruth Koya amesema mpaka sasa uchimbaji wa visima virefu 11 katika eneo la Seed Farm-Magereza vinavotarajiwa kutoa lita milioni 24 kwa siku umekamilika kwa asilimia 100, hali kadhalika visima 18 majimoto na 12 Valesca-Mbuguni vinavotarajiwa kutoa lita milioni 119,000 kwa siku ukiwa umefikia asilimia 50.

Ujenzi wa jumla kwa vipengele vyote kumi na mbili unaendelea na kwa sasa umefikia kiwango cha asilimia 30 na unatarajiwa kukamilika ifikapo mwaka 2020.

Kukamilika kwa mradi huo kutaongeza uzalishaji wa maji kutoka wastani wa lita 40,000 kwa siku hadi lita 200,000 kwa siku, sanjari na kuongeza idadi ya wakazi wanaopata maji toka wastani wa watu 325,000 hadi kufikia watu 600,000 wakiwemo wastani wa watu 250,000 wanaoingia na kutoka jijini Arusha kila siku143,770 kutoka katika wilaya za Arumeru, Hai na Simanjiro.

Kitengo cha Mawasiliano,

Agosti 22, 2019