Habari

Imewekwa: Jul, 28 2021

Naibu Waziri aagiza Malipo ya mradi wa Mwanambaya Mkuranga Pwani yafanyike.

News Images

Naibu Waziri wa Maji, Mhandisi Maryprisca Mahundi (Mb) amemuagiza Katibu Mkuu Wizara ya Maji Mhandisi Anthony Sanga atoe fedha za malipo kiasi cha sh. milioni 700 zilizoombwa na Wakala wa Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) wilaya ya Mkuranga ili kukamilisha ujenzi wa tanki la mradi wa maji Mwanambaya.

Mhe. Naibu Waziri alitoa maagizo hayo wakati alipotembelea mradi wa chanzo cha maji Mwanambaya na tanki linalokusudia kusambaza maji kupitia mradi huo.

“Nisisitize kuwa miradi inayokusudia kutoa huduma kwa wananchi tunaendelea kuitolea fedha kwa awamu hadi ikamilike ili kutimiza lengo la serikali la kumtua mama ndoo kichwani na kuondoa kero ya ukosefu wa upatikanaji wa majisafi, salama na yenye kutosheleza.

Aidha, ameelekeza Mameneja wa RUWASA mikoa na wilaya kuhakikisha jumuiya za watumia maji wanapata watunza fedha makini waliosoma na kufaulu masomo husika ili kuwezesha utunzaji mzuri wa fedha za miradi ya maji.

Pia, ameelekeza RUWASA Mikoa na Wilaya kukamilisha miradi kwa wakati ili kuharakisha huduma ya maji kwa wananchi.

Kwa upande wake meneja wa RUWASA Wilaya ya Mkuranga, Maria Malale alisema ujenzi wa mradi Mwanambaya unagharimu bilioni 2.3 ambapo bilioni 1.1 amelipwa mkandarasi. Mradi unatarajia kuhudumia zaidi wananchi 8,000.

Alisema mradi umefikia asilimia 90 ,mkandarasi anaendelea na kazi licha ya kudai fedha milioni 700 ambayo wameshaiombea fedha kwa ajili ya malipo.

Mkuu wa wilaya ya Mkuranga, Hadija Ally alisema ipo miradi inayoendelea ambapo ikikamilika yote wananchi watanufaika kwa kiasi kikubwa .

Hadija alifafanua ,upatikanaji wa maji mjini ni asilimia 86 na vijijini ni 76.

Katika ziara hiyo ya kikazi ,MaryPrisca alitembelea na kukagua pia mradi wa maji Mkerezange ambao umekamilika na upo kwenye matazamio.

Kutazama video yake Bofya HAPA