Habari

Imewekwa: Jul, 20 2021

​Mradi wa maji wa Bilioni 17 DAWASA kukamilika Septemba 2021

News Images

Naibu Waziri wa Maji, Mhe. Mhandisi Maryprisca Mahundi ametembelea na kukagua maendeleo ya utekelezaji wa mradi wa maji wa Mlandizi, Chalinze Mboga. Mradi huu unatekelezwa kwa thamani ya shilingi Bilioni 17.8 Fedha za ndani za Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) na unatarajiwa kuzalisha maji kiasi cha lita milioni 9 na laki tatu kwa siku.

Kiasi hiki cha maji kitaweza kuhudumia jumla ya wakazi 122,000 wa maeneo ya mlandizi, chalinze hadi mji mdogo wa Mboga.

Mheshimiwa Naibu Waziri amewapongeza DAWASA kwa usimamizi mzuri wa fedha za ndani. Amesema lengo la serikali ni kuondoa changamoto za upatikanaji wa huduma ya majisafi na Salama kwa wananchi jambo ambalo DAWASA wanalitekeleza vizuri.

Amesisitiza umuhimu wa kuwa karibu na viongozi wa serikali wakiwemo wakuu wa Mikoa, Wilaya ha watendaji wengine wa serikali. Amesema viongozi wa Serikali wanapaswa kufahamu shughuli mbalimbali zinazofanywa katika Sekta ya maji hivyo watendaji wahakikishe wanawatembelea na kuwajulisha hatua mbalimbali za utekelezaji wa miradi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Miundombinu na Uwekezaji DAWASA, Mhandisi Ramadhani Mtindasi amesema Mradi huo unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi wa 9 mwaka huu na utatatua kero ya Maji kwa wananchi wa maeneo husika pamoja na Bandari Kavu ya Kwara, pia Mradi wa Reli ya Kisasa ya SGR eneo la Kwara.

Naye, Mbunge wa Jimbo la Chalinze, Mhe. Ridhiwan Kikwete amewataka DAWASA waharakishe utekelezaji wa mradi huo ili wananchi waondokane na changamoto ya majisafi na salama.