Habari
Wakazi Zaidi ya 64,000 Manyoni Kunufaika na Mradi wa Maji
Timu ya wataalamu kutoka Wizara ya Maji, Wizara ya Mambo ya Nje, wakandarasi pamoja na Afisa Balozi wa India nchini Tanzania, Rajnish Kumar, na Mwakilishi wa Serikali ya India kutoka Benki ya Exim, Bw. Ravi V. P. Singh imetembelea Mradi wa Maji wa Miji 28 uliopo Wilaya ya Manyoni kwa lengo la kujionea kazi ya utekelezaji wa mradi huo.
Serikali kupitia Wizara ya Maji inaendelea kutekeleza mradi huo katika Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni, unaohusisha uchimbaji wa visima, ulazaji wa bomba kuu, ujenzi wa mtambo wa kusukuma maji, ujenzi wa tenki lenye ujazo wa lita 2,000,000 pamoja na ulazaji wa mabomba ya usambazaji maji yenye urefu wa kilomita 31.
Kwa sasa, utekelezaji wa mradi huo umefikia asilimia 65 na unatarajiwa kunufaisha wakazi zaidi ya 64,000 mara utakapokamilika.
Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni, Mary Kanumba, amesema wananchi wana matumaini makubwa na mradi huo kutokana na uzalishaji wa maji wa sasa kutokidhi mahitaji yanayoongezeka sambamba na ukuaji wa idadi ya watu na makazi katika mji wa Manyoni, amezungumza katika ziara hiyo.
Aidha, ameiomba Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na Serikali ya India kuhakikisha mradi huo unakamilishwa kwa wakati kama ilivyopangwa kwa kuwa utakuwa na manufaa makubwa kwa Mji wa Manyoni na wakazi wake, akisisitiza kuwa mradi huo utaondoa kwa kiasi kikubwa changamoto ya huduma ya majisafi na salama.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Benki ya Exim ya India,. Ravi V. P. Singh, amesema kuwa Serikali ya India kupitia benki hiyo haitaweka kikwazo chochote katika kukamilika kwa mradi huo, kwani dhamira yao ni kuona mradi unakamilika kwa wakati na wananchi wanapatana kufurahia huduma ya majisafi na salama.
Naye Afisa Balozi wa India nchini Tanzania, Rajnish Kumar, amemtaka mkandarasi anayetekeleza mradi huo, Kampuni ya Mega Engineering and Infrastructure Limited, kuhakikisha kazi hiyo inakamilika mapema ifikapo Aprili 2026, tofauti na mwezi Julai kama ilivyoainishwa kwenye mkataba.

